Sababu za Kuongezeka Bei ya Soda Nchini



Dar es Salaam. Gharama za uendeshaji zimetajwa kuwa sababu ya kuongezeka bei ya soda aina ya Cocacola na Pepsi.

Vinywaji hivyo kwa muda mrefu vimekuwa vikiuzwa kwa Sh500, lakini sasa imeongezeka na kufika Sh600 kwa soda za ujazo wa mililita 300 na 350.

Mwananchi ina nakala ya waraka wa kampuni ya Cocacola Kwanza Limited kwenda wa wateja wake (wauzaji wa rejereja) ikieleza gharama za uzalishaji ndiyo sababu ya kuongeza bei.

Taarifa hiyo ilieleza: “Tunapenda kukutaarifu juu ya mabadiliko ya bei kwa soda zetu za ujazo wa mililita 300/350 RBG, mililita 500 RGB na mililita 300 PET kipotabo. Mabadiliko haya ya bei ni kwa mawakala, wauzaji wa jumla na rejereja, bei hizi mpya zitaanza rasmi 1/4/2022. Hii ni kutokana na gharama za uendeshaji wa biashara,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugezi wa ukuaji na maendeleo ya biashara, Josephine Msalilwa.


Katika Waraka huo, Msalilwa alisema kwa bidhaa nyingine katika ujazo tofauti zinazozalishwa na kampuni hiyo bei yake haitaongezeka. Gharama za uendeshaji zilizopanda hazikuelezwa katika waraka huo, lakini bosi wa kampuni mojawapo inayozalisha bidhaa za Cocacola nchini aliliambia gazeti hili kuwa bei imeongezeka ili walau kufidia sehemu ya gharama zilizopanda ndani ya kipindi cha miaka 10 ambayo bidhaa hiyo haijapanda bei.

“Bei ya soda haijaongezeka kwa zaidi ya muongo mmoja, lakini tunapandisha mishahara ya wafanyakazi kila mwaka, viwango vya ubadilishaji wa fedha yetu kwa dola vinaongezeka kila mwaka na mali ghafi ambazo tunanunua kwa ajili ya kutengeneza soda zinanunuliwa kwa dola,” alisema.

Kiongozi huyo alisema kwa muongo mmoja ambao hawajaongezeka bei ya bidhaa zao, bei ya sukari ya viwandani imeongezeka kwa asilimia zaidi ya 100, vipuri vya mashine vimepanda bei na gharama zote hizo zilikuwa zinabebwa na kampuni ili kuendelea kuuza kwa Sh500 lakini sasa haiwezi tena.


Licha ya soda aina ya Pepsi kuongezeka bei kutoka Sh500 na kuuzwa kwa Sh600 kwa wanunuzi wa rejareja, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Umma wa Kampuni ya SBC Tanzania Limited, Foti Gwebe-Nyirenda alisema: “Bei ya soda zetu haijaongezeka, haijabadilika, kama kuna mahali umeshuhudia hilo mimi sijui labda unitajie”.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad