Sakata la Mirathi ya Marehemu Mpakanjia kwa Wanaye Lamalizwa Mahakamani

 


Marehemu Mpakanjia enzi za uhai wake alizaa na marehemu Amina Chifupa mtoto aitwaye Abdulrahman.

Sakata la utata wa mgawanyo wa mali zilizoachwa na aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa nchini, Mohamed ‘Meddy’ Mpakanjia lililozua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii miezi kadhaa iliyopita, limemalizwa katika Mahakama ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Watoto watatu wa marehemu, akiwemo aliyezaa na marehemu Amina Chifupa, Abdulrahman Mpakanjia, wamekubali kupokea mgawanyo wa mali zilizoachwa na marehemu baba yao, baada ya awali kugomea mchakato huo kutokana na utata ulioibuka kuhusu thamani halisi ya mali zote zilizoachwa na marehemu.

Akizungumza na mwandishi wetu, kaka wa marehemu Mpakanjia, Abdul Mpakanjia amesema msimamizi wa mirathi ndiye aliyelipeleka suala hilo mahakamani baada ya watoto wa marehemu kuugomea mgawanyo wa awali wa mali hizo.


“Tatizo lililokuwepo ni kwamba kulikuwa na sintofahamu kuhusu kiwango halisi kilichoachwa na marehemu lakini baada ya mahesabu kufanyika mbele ya wanasheria, watoto na ndugu wote wameridhia mgawanyo huo kwa hiyo kinachofuatia kwa sasa ni utekelezaji,” alisema.

Akaongeza kuwa mali alizoacha marehemu ni pamoja na fedha taslimu ambazo tayari zimegawanywa sawa kwa watoto wote watatu, nyumba tatu zilizopo maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, kampuni tano pamoja na gereji ya magari iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wetu amemtafuta Abdulrahman Mpakanjia ambaye kama ilivyoelezwa ni mtoto wa marehemu Amina Chifupa, ambapo amekiri kumalizika kwa mgogoro uliokuwepo mahakamani na kueleza kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni kutekelezwa kwa maamuzi ya mahakama.

“Tunamshukuru Mungu suala limeisha vizuri kabisa, sisi watoto wote tumekubaliana na mahesabu yaliyowasilishwa mahakamani na tayari mgawanyo wa baadhi ya vitu umeshaanza na naamini utaisha salama ili kila mmoja aweze kunufaika kwa kile alichotuachia marehemu baba,” alisema Abdulrahman

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad