Lindi. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amezungumzia matumizi ya helkopta katika ziara ya kukagua uanzishwaji wa anwani za makazi, akisema inawamsha watu kufanya kazi.
Nape ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 14 akiwa mkoani Lindi katika mfululizo wa ziara zake mikoani ambako anakagua uwekaji wa anwani za makazi
Amesema kazi hiyo inakwenda vizuri, lakini baadhi ya maeneo wamejisahaulisha hivyo wakisikia kelele za helkopta wanaamka na kufanya kazi.
Kauli ya Waziri Nape inakuja wakati kukiwa na maoni tofauti kuhusu matumizi hayo ya helkopta, huku baadhi ya watu wakihoji matumizi mabaya ya fedha za umma.
Hata hivyo, kupitia ukurasa wake kimtandao Waziri huyo alihoji kuhusu wanaohoji matumizi ya chopa akisema wanapaswa kufikiria kuhusu gharama za magari na muda uliobaki kufikia mwisho wa kazi hiyo.
"Kelele zimekuwa nyingi, maneno mengi lakini watu wakisikia helkopa inapita wanauliza kuna nini huko kwa hiyo wanaamka na kuanza kufanya kazi, kwa hiyo sisi Wizara tunafurahi kuhusu jambo hili," amesema Nape.
Amesema kazi hiyo ni ya Rais mwenyewe kwa hiyo hakuna kufeli katika hilo na amewaomba watu wamsaidie Rais kufikia ndoto za Tanzania ya kidigitali hata kabla ya muda uliopangwa.