Salah Atoa Neno la Kwanza Baada ya Kutupwa Nje Kufuzu Kombe la Dunia



STAA wa Misri, Mohamed Salah, amesema bado anajivunia kikosi cha sasa cha taifa hilo licha ya kupata simanzi mfululizo dhidi ya Senegal kwa kufungwa kwenye fainali ya Afcon 2021 na kufungwa tena kwenye kufuzu Kombe la Dunia 2022.

Mafarao hao walipigwa kwa penalti mara mbili na Senegal ndani ya mwaka huu. Hilo limesababisha kocha Carlos Queiroz ajiuzulu, juzi.

Salah ambaye alimulikwa na tochi nyingi usoni alipokwenda kupiga penalti yake na kukosa, na baadaye kurushiwa makopo na mashabiki wa Senegal, amesema: “Niliwaambia kabla ya mchezo wa pili kuwa najivunia kucheza nanyi na ninyi ni miongoni mwa wachezaji wazuri ambao nimewahi kucheza nao.”

“Nimecheza na kizazi kilichopita cha akina Wael Gomaa na Mohamed Aboutrika, halafu nikacheza na akina Abdallah El-Said na kizazi kilichofuata. Na naweza kusema kwamba nina furaha na kizazi hiki.


 
“Najivunia kuwahi kucheza nanyi na kilichotokea kilikuwa nje ya uwezo wetu kwa sababu ni penalti, na ni kwa mara ya pili. Ilikuwa ni furaha kucheza nanyi hata kama nitaondoka au nitaendelea kucheza hapa.”

Alipokuwa akizungumza, waziri wa michezo, Ashraf Sobhi, akaingilia na kusema: “Utaendelea kucheza hapa.”

Kauli hiyo ya Salah inakuja baada ya Fifa kuanza uchunguzi wa malalamiko yaliyotolewa na Misri kuhusu mchezo huo.


Salah alilazimika kusindikizwa na walinzi kuingia vyumbani baada ya kuanza kurushiwa makopo na chupa. Misri pia wamesema walionyeshwa vitendo vya kibaguzi na wakati wakipasha misuli, walirushiwa makopo na mawe huku basi lao likishambuliwa kabla ya mchezo na kusababisha majeraha kadhaa ya wachezaji.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad