Shaffih Dauda Aikingia Kifua Simba SC, atoa ushauri


 

Wakati Simba SC ikionyesha kuwa katika hatua za mwisho za kukubalia kuutema Ubingwa wa Tanzania bara msimu huu 2021/22, Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Shaffih Dauda amejitokeza hadharani na kuikingia kifua klabu hiyo.


Simba SC imechwa kwa alama 10 dhidi ya Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 51, huku kila mmoja akicheza michezo 19.


Shaffih Dauda anaamini suala la Simba SC kuwa mbioni kuupoteza Ubingwa wao msimu huu sio tatizo, kwani sehemu ya malengo ya kuwa Bingwa ni pamoja na kusaka nafasi ya kushiriki Michuano ya Kimataifa, licha ya kuongeza idadi ya mataji.


Shaffih ameitetea Simba SC kwa kuandika makala fupi ambayo anaamini itawasaidia mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania kufahamu sababu za klabu kuwania Ubingwa wa Ligi pamoja na Kushiriki Michuano ya Kimataifa.


Shaffih ameandika: Ukiangalia sababu kubwa inayovisukuma vilabu vya nyumbani kushindania ubingwa wa Ligi Kuu ni ushiriki wa mashindano ya Afrika [Ligi ya Mabingwa Afrika].


Kwa maana hiyo ubingwa wa Tanzania kwa Simba ambayo hadi sasa inashiriki mashindano matatu [mawili ya ndani, moja la kimataifa], nafikiri hadi sasa Simba haina haja ya kupambana sana kuizuia Young Africans kuwa bingwa wa Ligi msimu huu!


Simba tayari ilishafanikiwa pale ilipofuzu Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa sababu baada ya hapo ilikuwa tayari imetengeneza uhakika wa timu mbili kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu unaokuja.


Nafasi ambayo Simba ipo kwenye Ligi ya NBC [nafasi ya pili] inaihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambapo Tanzania itaingiza timu nne kwenye mashindano ya CAF, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili nyingine kwenye Kombe la Shirikisho.


Kwa hiyo kwa sasa kipaumbele kingekuwa ni kuzidi kwenda hatua za mbele zaidi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.


Kama wanataka kombe la ndani basi waweke nguvu kwenye Kombe la Shirikisho la Azam Sports. Kwenye Ligi Yanga tayari imeshatangulia kwa tofauti ya points nyingi (10).


Kama lengo kubwa la kupambania ubingwa ni kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwa nafasi waliyonayo sasa hivi wanauhakika wa kushiriki tena Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa hiyo Simba hawana haja ya kupigana vita kubwa ya ubingwa wa Ligi.


Waweke nguvu kubwa kwenye kushindania ubingwa wa Kombe la Shirkisho Afrika lakini kama wanataka taji la ndani basi wawekeze kwenye Kombe la Shirikisho la Azam Sports

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad