Simba Kusuka au Kunyoa leo, Rekodi Zambeba Simba Kwa Mkapa



​​​​​​​NI kusuka au kunyoa leo kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Simba wanaotakiwa wapate ushindi wa aina yoyote ile dhidi ya US Gendermerie ya Niger ili kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wachezaji wa Simba (kutoka kushoto) Joshua Onyango, Peter Banda, Shomari Kapombe na Bernard Morris wakiwa kwenye mazoezi kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendermerie ya Niger, utakaopigwa leo uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. PICHA: SIMBA
Mechi hiyo inachezwa majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ikicheza pamoja na mechi kati ya RS Berkane ya Morocco dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast ili kuondoa uwezekano wa kupanga matokeo, lakini kwa saa za Morocco itakuwa ni saa mbili usiku.

Itakuwa ikicheza mbele ya mashabiki wake wapatao 35,000 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao umekuwa ukiwapa ushindi kwa asilimia nyingi pale kwenye mechi za kuamua.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco amesema wachezaji wake wako katika hali nzuri ya kupambania timu na Tanzania kwa ujumla kwa ajili ya kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana.

"Nafahamu ugumu tutakaokutana nao kwa sababu US Gendermerie siyo timu ya mzaha, lakini niwaondoe hofu mashabiki wa Simba, kwani wachezaji hawatobweteka, kila mmoja anatakiwa kupambana ili kutimiza ndoto ya kutinga hatua hiyo," alisema kocha huyo ambaye kikosi chake kilitoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya timu hiyo Februari 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jenerali Seyni Kountche nchini Niger.


Juzi, Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji aliwatembelea kambini wachezaji wa timu hiyo na kuongea nao, kuongeza bonasi ili kuwafanya wapambane kwa ajili ya kufanikisha ushindi ambao licha ya kuifanya Simba kutinga hatua ya robo fainali, utaifanya Tanzania kupeleka moja kwa moja timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, naye wiki nzima amekuwa kwenye pilikapilika ya kuhamasisha mashabiki kuelekea kwenye mechi hiyo, pamoja na kujumuika na wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwenye stendi ya Magufuli maeneo ya Mbezi Louis, ambapo vikundi mbalimbali vya ngoma kutoka matawi kadhaa Dar es Salaam na Pwani, vilikutana.

Kuelekea kwenye mechi hiyo, pia alifanya ziara ya kupanda treni ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Pugu na kurejea tena, ambapo akiwa ndani alipata fursa ya kuzungumza na mashabiki kwa ajili ya kuwahimiza wajitokeze na kuwapa hamasa wachezaji.

Alijumuika pia na wasanii wa bongo fleva na filamu ambao ni wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa ajili ya kuamsha hamasa.

Simba inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi D kwa pointi saba na inahitaji ushindi ili kwenda robo fainali na timu yoyote itakayoshinda kati ya RS Berkane au Asec Mimosas, kwani itakuwa na pointi 10.

Iwapo Simba itatoka sare yoyote kwenye mechi ya leo na kufikisha pointi nane, basi itakuwa inaombea Asec Mimosas ishinde kwani itafikisha pointi 12 na kuiacha RS Berkane na pointi zake saba.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad