BAADA ya kutinga hatua ya robo fainali kwa kishindo usiku wa kuamkia jana, wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu, Simba, wameangukia mdomoni mwa vinara wa makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mshambuliaji wa Simba, Chris Mugalu, akishangilia baada ya kuiandikia timu yake bao la tatu wakati ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya US Gendarmerie na kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi. Anayeshangilia nyuma ni Shomari Kapombe. PICHA: SIMBA
Simba ambayo juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa iliichapa US Gendarmerie ya Niger kwa mabao 4-0, ushindi huo umeiwezesha kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D la michuano hiyo, ikiwa na pointi 10 sawa na vinara RS Berkane ya Morocco ambayo siku hiyo nayo iliichapa Asec Mimosas ya Ivory Coast bao 1-0.
Katika makundi mengine ya michuano hiyo ya CAF, Kundi A vinara ni Al Ahly Tripoli ya Libya iliyomaliza na pointi 13 sawa na Pyramids ya Misri iliyoko nafasi ya pili, wakati Kundi B, likiongozwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini yenye alama 13 ikifuatiwa na Al-Ittihad ya Libya yenye pointi 11 huku Kundi C, TP Mazembe ikiongoza kwa alama zake 11, moja mbele ya Al Masry ya Misri iliyomaliza ya pili.
Droo ya hatua ya robo fainali inatarajiwa kuchezeshwa leo Makao Makuu ya CAF jijini Cairo, Misri kabla ya mechi za hatua hiyo kupigwa Aprili 17, mwaka huu kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo upangaji wa droo utazingatia timu zilizotoka kundi moja hazitakutana katika robo fainali, lakini mshindi wa kwanza katika kila kundi atakutana na mshindi wa pili kutoka kundi lingine.
Hivyo, Simba ambayo imeshika nafasi ya pili kutoka Kundi D, katika droo hiyo ya leo, uwezekano uliopo ni kukutana na Al Ahly Tripoli, Orlando Pirates ama TP Mazembe ambazo ni vinara wa Kundi A, B na C, wakati RS Berkane kinara wa Kundi D, yenyewe inaweza kuangukia mdomoni mwa Pyramids, Al-Ittihad au Al Masry zilizoshika nafasi ya pili kutoka Kundi A, B na C.
Kuelekea droo hiyo leo, baada ya ushindi wa jana, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana mwanzo mwisho licha ya kupoteza nafasi nyingi kipindi cha kwanza, lakini akawapongeza mashabiki kwa kujitoa usiku kwenda kuishangilia timu yao.
Hata hivyo, Pablo alisema hatua inayofuata ya robo fainali itakuwa ngumu zaidi kwa kuwa watakutana na timu bora zilizomaliza nafasi ya kwanza katika makundi yao, hivyo wataenda kujipanga kukabiliana na ushindani watakaokutana nao.
"Niwapongeza wachezaji wangu kwa namna walivyojitoa na kujituma, pamoja na mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani usiku wa leo [juzi] kuisapoti timu licha ya mchezo kuanza katika muda ambao haukuzoeleka.
"Tunakwenda sasa kukutana na timu bora zilizoongoza makundi zenye uzoefu mkubwa, tunatambua itakuwa mechi ngumu zaidi, lakini Simba pia ni timu kubwa tutajipanga," alisema.
Hata hivyo, baada ya kikosi chake kumaliza nafasi ya tatu kikiwa na pointi tisa, Kocha Mkuu wa Asec Mimosas, Julien Chevalier, amesema Kundi lao la D, ndilo lilikuwa na timu bora zaidi, hivyo kutokufuzu kwao hakuna maana kwamba walizembea.
Akizungumza baada ya mechi yao dhidi ya Berkane kumalizika juzi nchini Morocco, Chevalier alisema timu zilizopita katika Kundi D, huenda bingwa akatokea hapo iwe Simba ama Berkane kutokana na ubora wao.
Kwa kutinga robo fainali, timu zote zilizoingia hatua hiyo, kila moja italamba Dola za Kimarekani 350,000 sawa na Sh. milioni 809.6 za Tanzania huku zilizoishia hatua ya makundi kwa kushika nafasi ya tatu na nne katika kila kundi, kila moja ikiondoka na Sh. milioni 632.
Timu zitakazofuzu nusu fainali zitaondoka na Sh. bilioni moja, wakati bingwa wa michuano hiyo akiondoka na Sh. bilioni 2.8 na mshindi wa pili Sh. bilioni 1.4.