SIMBA wajanja sana. Baada ya kusikia, mechi yao ya awali ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Sauzi itakuwa na VAR, fasta mabosi wa timu hiyo wameamua kuwapiga msasa mastaa wake, ili kukwepa mtego wake.
Simba na Orlando zitavaana Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mitambo ya VAR (teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi) inatarajiwa kufungwa leo kabla ya kutestiwa kesho kwa saa nne.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kuchezwa nchini kwa kutumia teknolojia hiyo, ikiwa imeanza kutumika kwa misimu michache sasa katika ligi kubwa nchini Ulaya, pia ikiwa imetumika katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 kule Cameroon.
Kwa Tanzania, hii ni mara ya kwanza na mastaa wa Simba kwenda kukutana na changamoto hiyo inayoweza kuwa faida kwao ama hasara kubwa kama hawatakuwa makini katika pambano hilo ambalo marudio yake yatafanyika wiki ijayo kule Sauzi.
Kutokana na ugeni huo, uongozi wa Simba umefichua una sababu za msingi kutoa semina kwa wachezaji wake watakaocheza mchezo huo wa kwanza utakaokuwa ukitazamwa katika kila tukio lao, hata lile ambalo litafanyika bila mpira uwanjani.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyimamu aliliambia Mwanaspoti jana kuwa watafanya semina ya kawaida kuwakumbusha nyota wao kujiandaa na mfumo wa VAR ambao watautumia kwa mara ya kwanza Jumapili.
“Kinachotakiwa kuongezeka ni umakini kwao, ingawa sheria za soka ni zile zile, isipokuwa kuna vitu ambavyo havitaonwa na mwamuzi, ila vitaonekana kutumia VAR, hivyo tutakumbushana ili wajiandae kwa hilo,” alisema Rweyemamu.
Mashabiki wa Simba watakuwa na furaha ikiwa timu yao itaibuka na ushindi kama ilivyozoeleka, lakini wasitarajie kuwa VAR inaweza kuwa upande wao pekee kutokana na uamuzi wake.
Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema VAR inamnufaisha zaidi mwamuzi kufanya uamuzi sahihi tofauti na kwa wachezaji.
“Kuna haja sasa ya wachezaji wa Simba, hasa mabeki kujiandaa kisaikolojia katika uamuzi wa VAR, kwani kwa namna moja au nyingine inaweza kuwa na madhara kwao, alisema Mayay na kuongeza; “Nasema hivyo kutokana na ukweli bila VAR makosa mengi huwa hayaonekani, lakini sasa mwamuzi atajiamini zaidi na kufanya uamuzi sahihi kwa sababu ana usaidizi wa video.”
Alisema wachezaji wa Simba wajiandae kisaikolojia na kujipanga kutofanya makosa ambayo yatawagharimu hasa safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikifanya makosa mengi zaidi.
Katika mchezo huo wa Jumapili, Simba itashuka bila nyota wake muhimu wa kikosi cha kwanza, Joash Onyango na Sadio Kanoute kutokana na kuwa na kadi tatu za njano. Nyota hao wanaweza kutumika katika mchezo wa marudiano wa Aprili 24, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Orlando, mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
MATUKIO YA VAR
Kama ilivyo kwa jina lake, VAR itaamua matukio ya msingi ambayo hayakuonekana na mwamuzi, kama utata wa bao, utata katika penalti, kadi nyekundu za moja kwa moja ama kuna makosa katika utoaji wa kadi.
Teknolojia hiyo ina uwezo wa kumwonyesha mwamuzi kuwa huenda alitoa kadi nyekundu kimakosa na kumshauri akatazame upya tukio lililosababisha kadi hiyo.
Tukio jingine la utata ni kuhusu kuotea, waamuzi wasaidizi wanashauriwa kuacha mchezo uendelee kama wanahisi tukio la kuotea limewapita, lakini shambulizi hilo likizaa bao, litatazamwa upya.
Hili linaweza kuwa tatizo kwa wachezaji wengi wanaotumia VAR kwa mara ya kwanza kwa kujisahau katika matukio ambayo nao wanadhani ni ‘offside’ na kuacha kukaba na kunyoosha mkono pekee.
Meneja wa Uwanja wa Mkapa, Gordon Nsajigwa alisema watu wa CAF, wenye utaalamu wa kufunga VAR wameshatua.
“Itafungwa na itatestiwa kwa saa nne,” alisema.