LICHA ya ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Orlando Pirates katika mechi ya robo fainali ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Klabu ya Simba imekiri itakuwa ni mechi ngumu kwao kuweza kufurukuta mbele ya miamba hiyo ya Afrika Kusini ikiwa uwanja wao wa nyumbani Jumapili.
Katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilipata bao hilo pekee dakika ya 67 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Shomari Kapombe baada ya Bernard Morrison kuangushwa ndani ya eneo la hatari, hivyo ili kufuzu nusu fainali sasa inapaswa kupata ushindi wowote ama sare yoyote.
Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, ameliambia Nipashe kuwa anafurahia matokeo hayo, lakini bado ana kazi kubwa ya kuimarisha mabeki wake kuhakikisha wanalinda ushindi wao katika mchezo wa marudiano nchini Afrika Kusini.
Pablo alisema ushindi huo umewapa faida kwenye mchezo wa marudiano ugenini Jumapili wiki hii, na kwamba wanatarajia kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Orlando Pirates, lakini watajipanga kuhakikisha wanaenda kufanya vizuri.
Alisema mabeki wanatakiwa kuwa imara kwa sababu ushindi waliopata nyumbani uko katika karatasi na vijana wake kutakiwa kubadilika hasa wanapokwenda kucheza ugenini.
“Lazima tubadilike, tunahitaji kwenda kuonyesha ushindani katika mchezo wa ugenini kuhakikisha tunaenda kuzuia na kutafuta bao la mapema katika mchezo huo wa marudiano.
“Hatukuwa na matokeo mazuri kwenye mechi za ugenini katika hatua ya makundi, hivyo tunapaswa kujipanga na kuwa imara katika safu ya ulinzi hasa kutokana na ubora wa wapinzani,” alisema na aliongeza:
“Michuano ya Afrika mara nyingi timu zinafanya vizuri nyumbani kama tulivyofanya, tutajipanga kuelekea mchezo wa marudiano ugenini kwa kuwa tunahitaji kufuzu nusu fainali,” alisema Pablo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again', naye amekiri kuwa ni kazi ngumu kuitoa Orlando Pirates kwenye hatua hii ya robo fainali, hivyo kazi kubwa ya ziada inabidi ifanyike kwao kama viongozi, benchi la ufundi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwenye mechi ya marudiano.
Akizungumza baada ya mchezo huo wa juzi, Try Again alisema ushindi wa bao 1-0 ni faida kwa Simba na muhimu, lakini wamepata ushindi mwembamba, hivyo inabidi kufanya kazi ya kuanza kuitoa timu hiyo kwao.
"Ni ngumu kushinda mabao mengi, fuatilia timu zote zilizocheza kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho, hakuna timu iliyoshinda mabao mengi, ushindi ni ushindi ingawa ni mwembamba, kwa sasa tunatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuitoa. Hii sasa ni mipango ya mwalimu na sisi viongozi kuangalia ni jinsi gani tunaweza kwenda kupata sare ugenini au kushinda, kikubwa ni kulinda ushindi wetu.
"Siwezi kusema lolote kuelekea mechi ya marudiano kwanza mpaka viongozi tukae na mwalimu, menejimenti na wadau kuangalia ni namna gani tutafanya kwa ajili ya mechi hiyo. Orlando ni timu nzuri na ina nidhamu, ilituheshimu kwenye mechi hii, tukapata penalti tukaitumia. Simba ni timu kubwa, kwenye hili tunaweza kupita na kusonga mbele kwenye michuano hii," alisema.
Baada ya mechi hiyo wachezaji wa Simba walipewa mapumziko ya siku moja na leo Jumanne watarejea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo wa marudiano.
Kwa uapnde wa Kocha wa Orlando Pirates, Mandla Ncikazi aliwapongeza Simba kwa ushindi waliupata na kucheza mpira wa ushindani mkubwa katika mchezo huo, lakini akalalamikia penalti haikuwa halali na wao kunyimwa penalti pamoja na mapokezi mabaya waliyoyapata.
“Simba hahitaji msaada wa waamuzi, timu nzuri ina wachezaji wazuri akiwamo Pape Sakho, Shomari Kapombe, Bernard Morrison, Mohammed Hussein, Taddeo Lwanga na Chris Mugalu,”alisema Ncikazi huku akimtupia mwamuzi wa mchezo huo, Haythem Guirat kutoka Tunisia kwa kuwapa Simba penalti na wao kunyimwa baada mchezaji wao kuangushwa ndani ya 18.