Simba imezima uvumi uliowashtua mashabiki wake juu ya mastaa wake watano kukutwa na maambukizi ya Uviko-19.
Meneja wa Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally amesema bado hawajapokea majibu ya vipimo vya Uviko na kwamba taarifa hiyo haina ukweli.
Ally amefafanua zaidi akisema kikosi chao kilifanya vipimo hivyo jana jioni na kwamba utaratibu ni kuwa majibu yatatoka ndani ya masaa 24 kutoka muda ambao walipima.
"Tumechukuliwa vipimo jana jioni kwa timu nzima na ukiangalia saa yako utaona hata masaa 24 hayajafika," amesema Ally.
"Mashabiki wetu wapuuze hizo taarifa waendelee kutuombea wakati huu tuko vitani tunatarajia majibu mazuri.
Aidha Ally ameongeza kuwa Simba inategemea majibu hayo kutoka leo baadaye na kwamba wameshachukua tahadhari zote za hujuma katika mambo yote
Katika taarifa ambayo imekuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii inadai kipa Aishi Manula,mabeki Shomari Kapombe,Mohammed Hussein 'Tshabalala' ,Joash Onyango na mshambuliaji Pape Sakho wamekutwa na maambukizi ya Uviko 19 baada ya vipimo hivyo.
Simba itashuka Uwanja wa Orlando kumalizana na wenyeji wao Orlando Pirates kesho saa 1:00 usiku katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya Robo Fainali.