WAKATI wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu, Simba wakiendelea na maandalizi makubwa kuelekea mechi ya mkondo wa pili ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, uongozi wa 'Wekundu wa Msimbazi' hao, ...
umesema katu hautavumilia kashfa zilizotolewa na kocha wa wapinzani wao hao, Mandla Ncikazi.
Jumapili wiki hii Simba inatarajia kushuka dimbani nchini Afrika Kusini kwenye mechi hiyo ya mkondo wa pili dhidi ya Orlando Pirates, ikiwa na faida ya bao 1-0 ililolipata katika mechi ya awali iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili iliyopita.
Katika mechi hiyo Kocha wa Orlando, Ncikazi, alitoa shutuma nyingi dhidi ya Simba baada ya kupoteza mchezo huo, akidai timu yake kupata mapokezi mabovu, huku pia akiilaumu kwa kushinda kwa mgongo wa waamuzi.
Hata hivyo, Ncikazi alipata mapokeo tofauti kwa mashabiki wa Orlando nchini Afrika Kusini, wengi wakiponda uwezo wake mdogo wa kuifundisha timu hiyo na kuutaka uongozi wa timu hiyo kumtimua yeye na kocha mwenza, Fadlu Davids.
Pamoja na 'misumari' hiyo ya moto ambayo Ncikazi anaipata kutoka kwa mashabiki wa Orlando, uongozi wa Simba umekemea vikali kauli zake na kueleza kusikitishwa kwani si za kiunamichezo na ni kinyume na kaulimbiu ya mchezo wa kiungwana (Fair Play), huku ukiweka wazi dhamira yake ya kulifikisha suala hilo kwa wenye dhamana ya mashindano hayo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
"Simba imechukizwa na maneno ya kashfa yaliyotolewa na Kocha Ncikazi ambayo yanatanabaisha ukosefu wa taaluma na ukiukwaji wa maadili katika kazi yake ya ukocha, ambayo yanakinzana na ukweli ambao Simba tumekua tukiiushi kwa kutoa huduma bora kwa wageni wote wanaokuja kucheza nasi hapa Tanzania.
"Simba tulishangazwa na vitendo vya Orlando tangu kuwasili kwao Tanzania ambapo kama wenyeji tuliandaa mazingira yote rafiki kwa ajili yao ikiwamo usafiri wa basi kubwa, na gari ndogo lakini kwa sababu zao walikataa kutumia huduma tulizowaandalia," ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez.
"Vilevile tuliwashauri kukaa hoteli ya karibu na mji, lakini kwa matakwa yao walichagua kukaa nje ya mji ambapo ni mbali na uwanjani hali iliyosababisha kuchelewa mazoezi kwa zaidi ya saa moja, lakini pamoja na hayo maofisa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa waliwaruhusu kufanya mazoezi licha ya kuwa muda kikanuni kwa timu kufanya mazoezi ulishamalizika. Ajabu ni kwamba Kocha Ncikazi hayaoni yote haya na kuamua kuipaka matope klabu yetu ambayo tunajivunia ukarimu na uungwaana kwa wageni wetu wote."
Aidha, ilieleza kuwa katika kile kinachoonekana kuwa Orlando walidhamiria kufanya vurugu Tanzania siku ya mchezo huo, waligoma kutumia mlango rasmi wa kuingilia vyumba vya kubadilishia nguo na badala yake wakatumia mlango wa kuingilia chumba cha mikutano cha wanahabari ambapo kiuhalisia si tabia ya timu kubwa.
"Kufuatia kashfa hizo zilizotolewa na Ncikazi, klabu ya Simba itawasilisha malalamiko rasmi kwenda kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na kupitia balozi za nchi zote mbili kuelezea yale yote yaliyoelezwa na kocha huyo.
"Katika nyakati hizi ambazo tunajiandaa na mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Aprili 24 ,mwaka huu, tunaiomba Serikali ya Tanzania na Serikali ya Afrika Kusini kutupatia ulinzi tukiwa safarini na tukiwa Afrika Kusini," ilieleza.
Aidha, Simba imekumbushia uhusiano mzuri wa kihistoria kati ya Afrika Kusini na Tanzania tangu enzi za ubaguzi wa rangi nchini kwao ambapo Tanzania ilikuwa sehemu ya kuwasaidia wapigania uhuru wa nchi hiyo kupambana na udhalimu waliokua wanafanyiwa watu wa Afrika Kusini, jambo ambalo kwa kashfa za Ncikazi zinaonesha wazi kuwa hajui lolote kuhusu uhusiano chanya uliopo baina ya pande hizi mbili