Simba, Yanga wakubali matokeo ya uwanjani





MIAMBA ya soka nchini Simba na Yanga itashuka Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam muda mfupi ujao mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba na Yanga ni kati ya mechi zenye upinzani, msisimko na mshawasha mkubwa kupita zote katika eneo hili la Afrika Mashariki na Kati.

Ni mechi inayokutanisha mahasimu wa jadi kwenye soka, wenye tabia na tamaduni tofauti kabisa na zile ambazo wengi wamezizoea katika maisha ya soka la timu pinzani za kawaida.

 Kwa kawaida upinzani wa soka wa timu pinzani za kawaida unakuwepo kwa takribani zile dakika 90 pale kiwanjani na zaidi ya hapo ni maisha ya kawaida kuchukua nafasi yake, lakini kwa hapa kwetu mara timu hizi zinapokutana kunakuwa na uhasama kuanzia nje na wakati mwingine hadi ndani ya uwanja.


 
Simba na Yanga daima ni mechi inayotawaliwa na maneno yanahusu ushirikina, hujuma, fitina, rushwa na kutokuaminiana kwa kiasi kikubwa kati ya mshabiki na mshabiki, kiongozi na kiongozi, wachezaji na mashabiki, viongozi na wachezaji.

Wakati mwingine hali inakuwa mbaya kufikia hata mchezaji na mchezaji kutokuaminiana kabisa na pengine kuangushiana shutumu za aidha kutaka au kuhujumu kabisa mechi hiyo.

 Ni kawaida kusikia baadhi ya wachezaji wa Simba,wakishutumiwa kuwa ni wapenzi au washabiki wa Yanga na hali kadhalika ni kawaida kusikia baadhi ya wachezaji wa Yanga, wakipata shutuma za wao ni Simba damu.


 Yatakayotokea leo uwanjani wakubaliane nayo, kama kuna timu itaenda uwanjani ikiamini itapata matokeo na haitakuwa hivyo, basi wakubaliane na kitakachotokea.

Umefika ushabiki kati ya timu hizi mbili ubadilike na uwe kimchezo zaidi,  ili kusaidia kuboresha soka letu, badala ya kuwa wa kiuadui.

Tatizo kubwa la washabiki wa mpira hasa wale Simba na Yanga, wenyewe hawaangalii mpira, wala hawakubali uwezo wa timu pinzani zaidi ya kama ni shabiki wa Yanga, kuing’ang’ania Yanga yako na kama ni Simba kufa na Simba yako.

 Wenzetu wanakubali uwezo wa timu nyingine na kuwapo changamoto wachezaji na viongozi, ili kuboresha viwango vyao na kuwapa raha washabiki wao.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad