Simbachawene anavyopenya kila mabadiliko ya mawaziri




 Simbachawene imeendelea kung’aa katika Baraza la Mawaziri baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko madogo, huku mwanasiasa huyo akiguswa katika kila mabadiliko yanayofanyika.

Wachambuzi wa siasa wamesema Simbachawene ni waziri kiraka mwenye uwezo wa kukaa katika wizara yoyote na kubadilishwa kwake wizara bila kuondolewa ni ishara kwamba Rais anaamini uwezo wake.

Juzi, Rais Samia aliwabadilisha wizara baadhi ya mawaziri wake ambapo Simbachawene ambaye alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, alipelekwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) wakati Pindi Chana, aliyekuwa katika wizara hiyo akienda Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk Damas Ndumbaro, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, sasa anakwenda Wizara ya Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Simbachawene.


 
Simbachawene amekuwa akiguswa na mabadiliko yanayofanywa na Rais tangu wakati wa Serikali ya awamu ya tano ya hayati John Magufuli, na wakati wote amekuwa akivuka salama wakati wengine wakiachwa.

Rais Samia alipofanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri muda mfupi baada ya kuapishwa, alimbakisha Simbachawene katika Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo aliteuliwa na hayati Magufuli Desemba 5, 2020.

Hata hivyo, Januari 8 mwaka huu, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya mawaziri na kumhamisha waziri huyo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda Wizara ya Katiba na Sheria, akichukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi.


Sifa za ziada

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alimuelezea Simbachawene kama mtu mwenye sifa za ziada.

“Taswira ya kwanza ni kwamba Simbachawene ni kiraka ambaye anaweza kuziba popote, maana yake ni kwamba ana sifa za ziada ambazo wakubwa zake wanaomteua wanaona ndani yake, ndiyo maana amekuwa akizunguka sana kwenye wizara mbalimbali.

“Anaweza akaingia kwenye wizara nyingi na akaweza kufanya kazi aliyopangiwa kufanya kwa ufanisi na pengine bila kulalamikiwa au kuleta kelele,” alisema

Katika Serikali ya awamu ya tano, mbunge huyo wa Kibakwe aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Januari 23, 2020 akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).


 
Mabadiliko hayo yalitokana na uamuzi wa Rais wa awamu hiyo kutengua uteuzi wa Kangi Lugola kutokana na kashfa ya mkataba wa ununuzi wa vifaa vya uokoaji uliokiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Simbachawene aliteuliwa katika nafasi hiyo ikiwa ni miezi sita tangu arejeshwe ndani ya Baraza la Mawaziri, baada ya kuwa nje tangu mwaka 2017 alipolazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya mikataba mibovu na uendeshaji wa biashara ya madini.

Shinikizo la kujiuzulu lilitokana na ripoti zilizotolewa Septemba 7, 2017 za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi zilizoonyesha namna Serikali ilivyopoteza trilioni za fedha kutokana na mikataba mibovu, baadhi ikiwa imesainiwa wakati akiwa Waziri wa Madini katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne.

Baada ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Rais Magufuli alitaka wote walioguswa kujiweka pembeni ili kupisha uchunguzi na Simbachawene, wakati huo akiwa Waziri wa Tamisemi, aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo.


Akiwa na mtazamo kama wa Dk Loisulie, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Frank Kimaro alisema kuendelea kubaki katika Baraza la Mawaziri, kunamaanisha Rais ana imani na utendaji wake.

“Waziri Simbachawene ameonyesha uwezo wake wa kufanya kazi kama kiraka, ndiyo maana ametumikia wizara mbalimbali na hakuna wizara ambayo imemshinda. Hiyo ni sifa yake kubwa,” alisema Kimaro.


Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad