Baadhi ya wakisubiri usafiri kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi jijini Dar es salaam huku wafanyabiashara nao wakiendelea na shughuli zao kituoni hapo. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Ni majira ya saa 4 usiku katika alama muhimu ya jijini Dar es Salaam, Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, ambacho muda huu kimeendelea kuwa mhimili wa shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara, mabasi kuingia kutoka mikoani na mengine kwenda maeneo tofauti kushusha abiria au kupakia mizigo.
Anayefika muda huu eneo hili hupata hisia kwamba mahali hapa watu hawalali kamwe, pengine hii ni ishara kuwa Dar es Salaam inaelekea polepole kuwa kitovu cha uchumi kinachofanya kazi kwa saa 24. Eneo maalumu la abiria katika kituo hicho limejaa watu, wengine wameketi, wengine wanajaribu kupata usingizi mwepesi, wengine wamelala sakafuni kwa sababu hakuna viti vingi vya kulalia.
Watu kama hao wengi wao ni wanaotarajia kusafiri mapema siku iliyofuata, huku wengine wakiwa tayari kusubiri ndugu zao wanaotarajiwa kuwasili kwa mabasi yanayofika jijini usiku wa manane kutoka sehemu tofauti ndani na nje ya nchi.
Lakini, wengine wasio na makazi wamegeuza kituo hicho kuwa makazi yao. Ingawa maofisa katika kituo hicho wanaeleza jinsi ilivyo vigumu kwa watu kuingia kwa siri na kufanya chumba cha kupumzikia cha abiria kuwa sehemu ya makazi na malazi, uchunguzi wa siku mbili wa gazeti hili unathibitisha wanafanya hivyo.
“Nitasafiri kwenda Zanzibar (nyumbani) kesho. Nilikuja hapa siku nne zilizopita kuchukua baadhi ya bidhaa Kariakoo na nimekuwa nikifanya hivyo kila siku na kurudi kulala hapa,” alisema Mohamed Mussa (35) aliyekutwa amelala kwenye stendi ambayo haitoi usafiri wa kwenda Zanzibar.
“Ni kweli nimeokoa zaidi ya Sh200,000, ambazo ningelipia malazi yangu sehemu nyingine, badala yake nimeongeza kwenye biashara yangu,” alisema mjasiriamali huyo kutoka Zanzibar.
“Niliweza kufanya hivyo kwa sababu hakuna mtu ambaye angegundua kuwa nilikuwa nikilala hapa usiku wote huo kwa sababu huwa natoka mahali hapa mara tu abiria wanapoanza kupanda mabasi,” alisema.
Ofisa mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu hana mamlaka ya kuzungumza, alisema aina ya usalama katika kituo hicho haiwezi kwa vyovyote vile kutoa nafasi kwa mtu au familia kufanya eneo hilo kuwa msaada kwao nyakati za usiku.
“Kila anayeingia katika kituo hicho ni lazima awe na tiketi inayoashiria kuwa atasafiri siku inayofuata na walinzi wanakagua kila mara. Wanaokamatwa bila tiketi huchukuliwa hatua za kisheria,” alifafanua.
stend pic 2
“Kituo hiki kinajulikana kuwa cha wasafiri, mtu yeyote anayeshughulikia tofauti lazima siku zake zihesabiwe...” alisisitiza. Hata hivyo, uchunguzi uligundua kuwa kufikia eneo la abiria ni rahisi kama utalipa ada ya Sh200 kwenye lango mojawapo katika kituo hicho.
Baada ya kufika kwenye kituo hicho usiku mmoja, kundi la wanaume wanne walimkaribisha mwandishi wa Mwananchi, wakitarajia ni mteja kwa siku inayofuata.
“Kaka unasafiri kwenda Arusha au Mwanza? Tiketi zipo,” mmoja wao alisema huku wakiendelea kumshawishi.
“Tuna viti vya kifahari, mabasi ya kawaida na ukitaka kusafiri usiku wa leo kuna mabasi binafsi pia ...”
Baada ya kulipa Sh300 kwenye lango kuu, kupanda ngazi hadi kwenye chumba cha abiria, watu wengi wanakutwa pale, wengine wamelala, wengine wakiendelea na biashara zao.
“Ulinzi wa hapa upo wa kutosha, hivyo watu wanaweza kulala bila tatizo na kila kukicha watu wanajazana hapa, kwani wengi hawaendi kulala hotelini kwa sababu ya gharama,” alieleza mlinzi mmoja ambaye pia aliomba kutotaja jina lake.
Kuanzia saa sita usiku hadi saa 8, mabasi yaliyosubiriwa kwa muda mrefu huanza kuwasili. Hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba hata baada ya waliofika wote kuondoka, eneo la abiria kwenye kituo hicho bado linaonekana limejaa, huku wauzaji wa vyakula na vinywaji wakiendelea na biashara zao.
“Baadhi ya watu wanaishi hapa, ingawa hairuhusiwi. Wapo ambao hawana makazi maalumu jijini Dar es Salaam, hasa wanaofanya kazi hapa kituoni,” alifichua mchuuzi mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa.
“Wamefanya mahali hapa kuwa makazi yao kwa kujifanya wasafiri. Hata hivyo, tuna furaha kwa sababu ni miongoni mwa wateja wetu wanaoaminika na hatuwezi kuwafichua pia kwa walinzi,” aliongeza.
Anatoa ishara kwa moja ya maeneo wanayolala watu kama hao. Baada ya kusogea karibu yao kwa mazungumzo huku wakijifanya wahitaji malazi kwa siku mbili walianza kufunguka.
“Kaka sisi tunalala hapa si kwa sababu tumeruhusiwa, tunatumia uwezo wetu tusijulikane. Tupo wengi, hivyo bora utafute hoteli nje,” alieleza mmoja wao huku wenzake wakimpa tahadhari dhidi ya walinzi ambao hawakuwa mbali sana.
“Mimi hupata takriban Sh10,000 kila siku hapa (kituoni). Ninatoka Iringa ambako nina familia inayohitaji msaada wangu. Sasa nikikodisha chumba, nitaweza kweli kuhudumia familia yangu? Ndiyo maana tunalala hapa kama abiria bila kutambuliwa,” alieleza.
Muuzaji wa vinywaji alisema kikundi hicho kilikiuka sheria kwa kuwa eneo hilo tayari limetangazwa kuwa la abiria na wale wanaosubiri kupokea wasafiri kutoka mikoani ili kupumzika ukumbini.
“Hapa ulinzi umehakikishwa na wale wanaolala hapa lazima wawe wajanja sana kwa sababu wakigunduliwa watashughulikiwa,” alifichua.
“Tunaona nyuso zilezile ambazo hulala hapa hata kwa wiki nzima kwani wanapata tu risiti za kuingilia ambazo zinagharimu Sh300 tu na sio tiketi ya kusafiria,” alibainisha. Mmoja wa walinzi, ambaye alisema alikuwa mkaguzi usiku huo, alisisitiza; “Ndugu nisikilize, hakuna mtu anayelala hapa bila tiketi ya kusafiria na wote wanaopokea wasafiri wanajitambulisha na kuondoka baada ya wageni wao kufika.”