KIUNGO wa Yanga, Salum Abubabakar 'Sure Boy' ameeleza furaha yake kurejea tena kwenye uwanja aliouzoea wa Azam Complex, Chamazi akiwa na timu yake mpya, huku akipata ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza mara baada ya mechi ya Ligi Kuu kati ya timu yake mpya ya Yanga na waajiri wake wa zamani, Azam FC, Sure Boy alisema ilikuwa ni mechi yenye hisia, kwani alikuwa akicheza dhidi ya timu iliyomlea, na timu yake mpya, pia kwenye uwanja ambao wameuzoea sana, ndiyo maana hata kiwango chake kilikuwa ni kikubwa.
"Tumepata pointi tatu, mechi ilikuwa ngumu, timu zote tulicheza vizuri, pale kati tulikuwa na kazi kwa sababu wote tulikuwa tunafahamiana, mimi nimecheza kwenye timu ya Azam na wachezaji waliokuwa wanacheza nafasi ya kiungo, kwa hiyo kila mmoja alikuwa anaonyesha nini anacho mguuni, si kweli kama tulikuwa tumekamiana sana kama baadhi ya watu wanavyosema. Wao wameuzoea uwanja na mimi pia nimeuzoea pia na tumezoeana hata mazoezi tulikuwa tunacheza wote, kwa hiyo ilikuwa ni kazi kubwa pale katikati, naamini tulicheza vizuri wote, mimi nilitaka kuonyesha vitu na wao hawakuniacha, ila hatukukamiana," alisema.
Sure Boy alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo la msimu huu, akitokea Azam, na haikuwa mara ya kwanza Yanga kufanya jaribio la kutaka kumsajili mchezaji huyo, ambaye mara kwa mara lilikuwa linagonga mwamba.
Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya kiungo, ni mtoto wa winga wa zamani wa Yanga, Aboubakar Salum, aliyetamba na timu hiyo akitokea Sigara, miaka ya katikati ya 1980 na kupewa jina la 'Sure Boy' ambalo mtoto wake kwa sasa analitumia.