Ule msemo usemao ‘vita vya panzi furaha ya kunguru’ umejidhihirisha ambapo Tanzania inatarajia kupata watalii wengi siku za hivi karibuni kutokea Urusi kutokana na nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Marekani.
Hayo yamebainishwa katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Fredrick Kibuta na Mbunge kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi, Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi.
“Kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Urusi, watalii wengi raia wa Urusi wanatarajiwa kuja Afrika ikiwemo Tanzania na kwamba Tanzania iandae mazingira wezeshi ikiwemo kuzingatia suala la usalama wa watalii”, alieleza Revaldovich.