Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Tigo, CPA Innocent Rwetabura (kushoto) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba baada ya kusainishana mkataba huo katika hafla iliyofanyika Jengo Jipya la PSSSF.
DAR ES SALAAM. Tarehe 27 Aprili, 2022. Kampuni inayoongoza kwa utoaji wa huduma za kidijitali nchini, Tigo Tanzania, imesaini mkataba wa kupangisha Jengo la PSSSF Tower Commercial Complex , kati ya MIC Tanzania PLC na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa nia ya kupanua wigo na kuharakisha utoaji wa huduma ambapo sasa watahama Jengo la Derm Complex kwenda ofisi kubwa jengo la PSSSF Floor ya 30 hadi 33 linalopatikana Kiwanja namba 3 , Barabara ya Sam Nujoma Sinza – Dar Es Salaam Tanzania.
Akizungumza kabla ya kusaini Mkataba huo CPA Innocent Rwetabura, CFO na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tigo amesema kuwa;
“Lengo la kuhamia katika jengo hili ambalo nimearifiwa kuwa ndio jengo refu kuliko yote Afrika ya Mashariki, ni kuziweka sehemu moja timu zilizounganishwa (Tigo/Zantel) ili kujenga mazingira bora yatakayochagiza umoja na ubunifu miongoni mwa wafanyakazi wetu ili kwa pamoja tuweze kutengeneza bidhaa na kutoa huduma za hali ya juu kwa wateja wetu zaidi ya million 14 kote nchini.
Tunatarajia kuanza kuhamia mwishoni wa mwaka huu wa 2022 na ofisi hizi mpya zitaakisi utamaduni wa taasisi iliyounganishwa (Tigo & Zantel) na tutajitahidi kuifanya iwe mahali pazuri pa kufanya kazi na kukuza vipaji vya ndani. Makazi haya mapya yanajumuisha vyumba vya mikutano vilivyowezeshwa na teknolojia na vituo vya kazi ambapo timu zinaweza kufanya kazi pamoja na wadau mbali mbali, washirika na wafanyakazi ambao wapo nje ya makao makuu hapa Dar es Salaam.
Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kubuni bidhaa na huduma zinazo walenga mteja mmoja mmoja pamoja na wateja wa makampuni makubwa na madogo. Nichukue fursa hii kuwahakikishia ya kwamba zoezi la kuhamisha makao makuu ya Tigo Tanzania kutoka jengo la Derm Complex Kijitonyama na kuja hapa PSSSF Commercial Complex hakutaathiri utoaji wa huduma zetu kwa namna yeyote ile”.
Pia, napenda kushukuru tena wenyeji wetu PSSSF kwa kutupa ushirikiano wa hali ya juu pamoja na kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa weledi mkubwa. Kwa namna ya pekee nichukue fursa hii tena kumshukuru kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kishimba, kwa kuwa nasi kila hatua na kuhakikisha tunafanikisha siku hii ya utiaji saini”. Alimalizia CPA Rwetabura.
Kwa Upande wake , Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, aliikaribisha Tigo Tanzania kwenye jengo hilo jipya, ambapo alisema;
“Tumefurahishwa sana na uamuzi wa MIC Tanzania PLC kuhamia Makao Makuu yake katika jengo ili la PSSSF Commercial Complex Sinza Karibuni sana, nina uhakika uwepo wenu hapa utafunga mikataba zaidi ya ukodishaji kwa PSSSF”.