Mtoto mwenye umri wa miaka minne mkazi wa Kijiji cha Lyabukande, Halmashauri ya Shinyanga amefariki dunia baada ya kupigwa fimbo na bibi yake kisha kumwagiwa maji ya moto kutokana na kujisaidia hovyo huku mdogo wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu akijeruhiwa kwa fimbo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga George Kyando, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 11:00 katika kijiji hicho baada ya bibi yao Tatu Moshi, kuwapiga kwa fimbo wajukuu zake wawili kisha kummwagia maji ya moto tumboni na miguuni mtoto mmoja na kusababisha kifo chake huku mwingine akijeruhiwa.
"Inasemekana amekuwa akiwaadhibu mara kwa mara wajukuu wake kwa madai kuwa wamekuwa wakijisaidia hovyo katika mazingira yake, hivyo amekuwa akiwaadhibu na kuwaachia majeraha mabaya katika miili yao, ukatili huu ni wa muda mrefu na majirani wanaona, na mama mzazi alikuwa anaona watoto wake wanafanyiwa ukatili lakini hawasemi hivyo mnatakiwa muondoe ukimya" amesema Kamanda Kyando.