Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv, Aprili 9, 2022.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv, Aprili 9, 2022. AP - Evgeniy Maloletka
Katika siku ya 46 ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 10 Aprili, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alifanya ziara ya ghafla nchini Ukraine ambapo alikutana na Rais Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alifanya ziara ya kushtukiza katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, mnamo Aprili 9, na kumfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa G7 kuzuru Ukraine tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake mnamo Februari 24. Boris Johnson aliahidi kuipatia Ukraine magari ya kivita na mifumo ya kujizuia na makombora pamoja na msaada zaidi wa kifedha na kutoa wito kwa nchi nyingine "kuiga mfano wa Uingereza".
Wakati huohuo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema taifa hilo limejiandaa kwa mapigano makali na vikosi vya Urusi vilivyojiimarisha mashariki mwa nchi hiyo huku Uingereza ikiahidi msaada mpya wa kifedha na kijeshi.
Takriban euro bilioni 10 zimekusanywa wakati wa kongamano la kimataifa la kuunga mkono Ukraine. Miongoni mwa pesa hizo zilizotolewa na Tume ya Ulaya, "euro milioni 600 zitaenda kwa mamlaka ya Ukraine na sehemu moja kwa Umoja wa Mataifa", alibainisha Ursula von der Leyen, ambaye alithibitisha kwamba euro milioni 400 zitalipwa kwa mataifa yalioko katika mstari wa mbele katika mapokezi ya wakimbizi.
Takriban watu 52 waliuawa na 109 kujeruhiwa katika shambulio la roketi kwenye kituo cha Kramatorsk huko Donbass, ambapo raia wanatoroka eneo hili la mashariki mwa Ukraine. Moscow imekanusha kuhusika shambulio hilo na kushutumu "uchochezi" wa vikosi vya Kyiv.