Umoja Party Waeleza Sababu Kutumia Picha ya Magufuli



Dar es Salaam. Mwanzilishi wa Chama cha Umoja Party Seif Maalim, amesema wameamua kutumia picha wa Hayati Rais John Magufuli katika fulana za chama hicho kwakuwa sera zao zinaendana na mlengo aliokuwa nao kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Chama hicho kimepeleka maombi ya usajili wa muda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ambaye jana amekionya kiache kufanya shughuli za kisiasa wakati si chama cha siasa kilichosajiliwa.

Katika mitandao ya kijamii zimesambaa picha zikiwaonyesha watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Umoja Party wakiwa wamevaa fulana zenye bendera ya chama hicho zikiambatana na picha ya hayati Magufuli.

Akizungumza na Mwananchi, Maalim ambaye pia alikuwa mgombea wa urais mwaka 2020 kupitia tiketi ya chama AAFP, amesema wametumia picha ya hayati Magufuli katika fulana zenye bendera ya chama chao kwa lengo la kujitangaza kwa wananchi.


“Kimsingi hatukuwa na nia mbaya kutumia picha ya hayati Magufuli ambaye si mwanachama wetu bali tumefanya hivyo kujitangaza kwa wananchi na kwa kuwa sera zetu zinalingana na kile alichokuwa akikisimamia” amesema

Maalim amesema kuwa wanaamini kuwa Ofisi ya Msajili itawaandikia barua itakayoonesha makosa yao na kuwaambia wapi wamekosea ili warekebishe kwa kuwa hawapingani na maelekezo ya msajili.

Barua ya msajili

Jana Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alitoa taarifa ya kuionya Umoja Party kwa kuanza kufanya kazi kabla ya kupata usajili wa muda huku akiweka wazi kufanya hivyo ni kukiuka utaratibu.


Katika maelezo yake, Nyahoza amesema kuna picha katika mitandao ya kijamii za watu wanaosekamana kuwa ni wanachama wa Umoja Party, wakionekana wamevaa fulana zenye bendera ya chama chicho, pamoja picha kiongozi ambaye sio mwanachama wao.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatumia fursa hii, kuwakumbusha wanaotengeneza, wanaovaa fulana hizo na Watanzania wote kuwa ni kosa la kisheria kwa taasisi yoyote kufanya kazi kama chama siasa wakati sio chama cha siasa kilichosajiliwa.

“Ni kosa kwa chama cha siasa kilichowakilisha maombi ya usajili wa muda, kufanya kazi kama chama cha siasa wakati hakijapewa cehti cha usajili wa muda kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa sura ya 258,” alisema Nyahoza.

Nyahoza amesema mtu yeyote anayefanya siasa kwa kutumia jina la ‘Umoja Party’, bendera, nembo au alama yoyote ya chama hicho, anakiuka sheria na anapaswa kuacha mara moja. Pia aliwataka waanzilishi wa Umoja Party kuendelea kufuatilia maombi ya usajili wa muda walioyawasilisha.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad