Leo Jumamosi kutakuwa na mchezo wa watani wa jadi katika Ligi kuu Tanzania Bara ambapo Yanga itaikaribisha Simba.
Simba katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao walikuwa wenyeji wa Yanga, matokeo yalikuwa 0-0. Tukienda kushuhudia mchezo wa mzunguko wa pili unaotarajiwa kufanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, Yanga wataingia wakiwa na pointi 13 zaidi ya Simba.
Kuelekea mchezo huo ambao umekuwa na mambo mengi ndani na nje ya uwanja, vijembe, tambo na hamasa zimeonekana kuwa kubwa katika upande wa wasemaji wa timu hizo.
Kwa upande wa Yanga, Haji Manara, ameanza tambo kuelekea mchezo huo kutokana na wao kuwa wenyeji. Simba wanaye Ahmed Ally, yeye ameanza kutamba kuwa lazima wapate matokeo dhidi ya Yanga.
Vita kubwa ambayo itakuwa inasubiriwa kuonekana ni kati ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na beki wa kati wa Simba, Henock Inonga Baka maarufu Varane. Vuta picha katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo namna Inonga alivyokula sahani moja na Mayele.
Katika mchezo huo, Mayele alikamatwa haswa na beki huyo ambaye wote wanatokea DR Congo. Wakati Mayele anafanyiwa mabadiliko, Inonga akamsindikiza na kuonesha ishara kuwa amemdhibiti mshambuliaji huyo kiasi cha kushindwa kutetema.
Mayele ambaye ni kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akiwa nayo 12, atakuwa na kazi moja ya kusaka rekodi ya kuwafunga Simba ndani ya ligi hiyo ikiwa tayari amewafunga Ngao ya Jamii. Mwenyewe ameweka wazi kwamba bado ana deni na Simba, hivyo amejipanga kulilipa. Hapo Inonga atakuwa na kazi kuhakikisha anamzuia tena asifunge.
Nani kusepa na POINTI 3 muhimu kati ya Yanga ama Simba⁉️ Dondosha utabiri wako...