MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi mkoani Morogoro.
CAG Charles Kichere.
Vilevile, amebaini kukosekana kwa uwazi katika mchakato wa ununuzi wa mtambo wa kuzalisha sukari kwa ajili ya kiwanda hicho na utata wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kupewa zabuni ya kununua na kufunga mtambo huo.
CAG Charles Kichere ametoa angalizo la kutokea hasara katika uwekezaji huo unaotumia fedha za wanachama wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 ambayo sasa iko wazi kwa umma baada ya kuwasilishwa bungeni wiki iliyopita.
Anafafanua kuwa Mkulazi ni kampuni tanzu ya NSSF (kwa asilimia 96) na Shirika la Magereza (asilimia nne) inayotekeleza miradi miwili ya viwanda vya sukari (eneo la Mkulazi na Mbigiri) vinavyolenga kuzalisha tani 250,000 za sukari kwa mwaka.
Anasema kwa mujibu wa Mpangomkakati wa Kampuni ya Mkulazi (2020/21 -2025/26) uliofanyiwa marekebisho, mradi wa Mbigiri ulitarajiwa kuanza uzalishaji msimu wa mwaka 2021 na kuzalisha tani 15,234 za sukari ifikapo msimu wa mwaka 2022.
"Mradi wa Mkulazi ulipanga kuanza uzalishaji katika msimu wa mwaka 2023 kwa makadirio ya uzalishaji wa tani 31,098 za sukari ifikapo msimu wa 2024.
"Hata hivyo, katika ukaguzi wangu, nilibaini hadi tarehe 26 Februari 2022, Kampuni ya Mkulazi ilikuwa haijakamilisha ufungaji wa mashine za kiwanda katika eneo la Mbigiri ambapo ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 13.8 na ujenzi wa miundombinu ya eneo la Mkulazi ulikuwa unaendelea.
"Kampuni ya Mkulazi ilinieleza kuwa kucheleweshwa kwa ufungaji wa mashine kiwandani kulisababishwa na mlipuko wa janga la UVIKO-19 lililoathiri kuwasili kwa mashine zilizonunuliwa nje ya nchi na kusafiri kwa washauri wa ufungaji wa kiwanda," anasema.
Vilevile, CAG alibaini kuwa kutokana na kuchelewa kwa ujenzi na ufungaji wa mashine za kiwanda cha sukari, Kampuni ya Mkulazi iliuza miwa iliyovunwa kwa sababu kiwanda hakikukamilika ili kuanza uzalishaji wa sukari.
Anabainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/21, kampuni ilivuna hekta 382 za miwa na kuuza tani 32,121.6 kwa Sh. bilioni 1.16.
UTATA UNUNUZI MTAMBOCAG pia anabainisha kuwapo udhaifu katika ununuzi wa mtambo wa kiwanda cha sukari katika Kampuni ya Mkulazi Holding Company Limited.
Anasema udhaifu huo unajumuisha ukosefu wa sababu za msingi za kuihusisha TANROADS katika ununuzi wa mtambo wa kiwanda hicho cha sukari.
CAG anaendelea kubainisha kuwa Menejimenti ya Kampuni ya Mkulazi haikutoa sababu za msingi za kuchagua TANROADS kufanya ununuzi kwa niaba yake na siyo taasisi zenye uzoefu wa ununuzi kwa niaba ya taasisi za serikali kama vile TEMESA au Wakala wa Ununuzi Serikalini.
"Pia nilibaini Kampuni ya Mkulazi haikutekeleza wajibu wake wa ununuzi kama ilivyokuwa imeelezwa kwenye makubaliano. Kwa mujibu wa nakubaliano, TANROADS alitakiwa kufanya mchakato wa ununuzi hadi zabuni itakapotolewa kwa mshindi wa zabuni na utiaji saini ulipaswa kufanywa na Kampuni ya Mkulazi.
"Hata hivyo, nilibaini kuwa TANROADS ilifanya mchakato mzima wa ununuzi. Hapakuwa na ushahidi kuwa Kampuni ya Mkulazi ilihusika katika kuandaa mahitaji, vipimo na makadirio ya majenzi (BOQ) kwa ajili ya kusanifu, kuleta, kusimika na kuuzindua mtambo wa kiwanda cha sukari (pamoja na kusafisha) kabla ya mwaliko wa zabuni kama ilivyoainishwa katika makubaliano," anafafanua.
UDHAIFU UTIAJI SAINICAG anasema kuwa wakati makubaliano yaliitaka Mkulazi kutia saini mkataba, alibaini kuwa makubaliano hayo yalifanyiwa marekebisho ili kuipa
TANROADS mamlaka ya kutia saini.Anabainisha zaidi kuwa Oktoba 23, 2019, TANROADS iliingia mkataba wa usanifu, kuleta, kuusimika na kuzindua mtambo wa kiwanda kwa bei ya mkataba ya dola za Marekani milioni 50.86 na Sh. bilioni 11.74 cha ziada ikiwa ni pamoja na kodi nyinginezo za ndani.
"Sikupata ushahidi kuwa mkataba ulihakikiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama inavyotakiwa na Kanuni ya 59(1) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013.
"Aidha, Kampuni ya Mkulazi haikuwa na jukumu la kusimamia huo mkataba na hivyo mradi unasimamiwa na TANROADS. Kwa hivyo, malipo kwa ajili hiyo hufanywa na NSSF baada ya kupokea hati na nyaraka za malipo kutoka TANROADS.
"Kutofuatwa kwa taratibu za ununuzi kulisababishwa na kukosekana kwa uwazi katika maandalizi ya zabuni, kuomba tathmini na kutoa zabuni kunakoweza kusababisha hatari, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mitambo isiyokidhi viwango vinavyotakiwa, kununua mtambo kwa bei kubwa, kuchelewa kuletwa kwa mtambo ulionunuliwa na hivyo kushindwa kupata thamani ya fedha katika mkataba huo,"anatahadharisha.
Katika hilo, CAG anapendekeza Kampuni ya Mkulazi kwa kushirikiana na TANROADS kuhakikisha utekelezaji wa mikataba unasimamiwa ili kuhakikisha mkataba unatekelezwa ndani ya muda uliopangwa, pia kuwa na taratibu zinazofaa za kutunza nyaraka za malipo ili kuweka uwazi kwa pande zote mbili.