MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini vifo vya wanyapori 614 kutokana na ajali za barabarani katika kipindi cha mwaka mmoja, sawa na vifo vya wanyamapori 51 mwezi.
CAG Charles Kichere anabainisha takwimu hizo katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 aliyoikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 30, mwaka huu kisha kuwasilishwa bungeni jijini hapa Jumanne iliyopita.
Anasema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia jumla ya hifadhi 22 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 104,170. Kati yake, ni Hifadhi za Taifa Mikumi, Serengeti, Tarangire na Ziwa Manyara.
CAG anasema Hifadhi ya Taifa ya Mikumi inapitiwa na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 45 huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikipitiwa na barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 12 ikitokea Mbalageti hadi Mto Robana.
"Ukaguzi wangu ulibaini kuwa katika mwaka 2020/21, wanyama 535 waliuawa kwenye ajali za barabarani katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kulinganishwa na wanyama 106 katika mwaka 2019/20.
"Idadi hii ni ongezeko la wanyama 429, sawa na asilimia 405. Wakati huohuo, nilibaini kuwa wanyama 50 waliuawa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti; wanyama 18 waliuawa katika Hifadhi ya Taifa Tarangire; na wanyama 11 waliuawa katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara.
"Kwa maoni yangu, ikiwa hatua madhubuti za usalama hazitachukuliwa kuzuia uzembe wa madereva ndani ya barabara zinazopita kwenye hifadhi za taifa, kuna uwezekano wa wanyamapori kuendelea kuuawa kwa ajali za barabarani.
"Ninapendekeza serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ipitie upya taratibu za uendeshaji salama wa magari ndani ya hifadhi za taifa nchini ili kudhibiti ajali zinazoua wanyamapori hifadhini," anatoa hoja.
UPUNGUFU WA FEDHA
CAG pia anasema amebaini upungufu wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika hifadhi za taifa. Anafafanua kuwa kabla ya mwaka 2020/21, mapato ya utalii yalikuwa yanakusanywa na TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), lakini kuanzia Julai Mosi, 2020, serikali iliagiza kisheria mapato hayo yakusanywe na Mamlaka ya Mapato (TRA) huku serikali ikiahidi kutoa fedha zinazohitajika kwa hifadhi hizo kulingana na bajeti za hifadhi hizo.
Hata hivyo, CAG anasema mapitio yake yalibaini tofauti kubwa kati ya bajeti zilizoidhinishwa kwa ajili ya hifadhi hizo na kiasi kilichotolewa na serikali kugharamia miradi ya maendeleo ya hifadhi husika.
"Kwa mfano, NCAA ilitarajia kupokea Sh. bilioni 31.21 kulingana na bajeti yake ya shughuli za maendeleo, lakini serikali ilitoa Sh. bilioni 10.27 tu, sawa na asilimia 33 ya bajeti iliyoidhinishwa. Hivyo, miradi iliyotekelezwa ilikuwa miradi 15 tu kati ya miradi 36.
"Pia, nilibaini kuwa kiasi hicho cha Sh. bilioni 10.27 kilichelewa kutolewa kwa muda wa miezi saba, ambapo mamlaka iliomba fedha hizo tarehe 21 Oktoba 2020 lakini serikali ilizitoa tarehe 5 Mei 2021.
"Kadhalika, nilibaini kuwa bajeti ya maendeleo ya TANAPA ilikuwa Sh. bilioni 69.52 lakini ni Sh. bilioni 26.51 tu, sawa na asilimia 38 ndiyo ziliidhinishwa kutolewa," anabainisha.
CAG ana angalizo kwamba kutolewa kwa fedha chini ya bajeti kulichangia kutotekelezwa kwa shughuli za maendeleo ya hifadhi zinazohusiana na miundombinu, uhifadhi, na huduma za utalii