Dar es Salaam. Maofisa wa Jeshi la Polisi zaidi ya 20 wanadaiwa kutapeliwa fedha kwa njia ya mtandao na mtu aliyejitambulisha kuwa na cheo cha Meja Jenerali wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutoka kitengo nyeti serikalini.
Tukio hilo linadaiwa kuwa la kwanza kutokea nchini na ukizingatia Jeshi la Polisi ndilo lenye dhamana ya kushughulika na uhalifu wa kimtandao, lakini inadaiwa mtuhumiwa huyo aliweza kujipenyeza kwa maofisa hao bila kugundulika na kufanikiwa kuwatapeli.
Vyanzo vyetu vimedokeza miongoni mwa wanaodaiwa kutapeliwa ni maofisa waliotaka kupewa wadhifa wa ukamanda wa polisi wa mikoa (RPC), waliotaka kupandishwa vyeo na waliotaka kuwa wakuu wa polisi wa wilaya (OCD) au kuhamishwa kituo kimoja kwenda kingine.
Mbali na kundi hilo, lipo kundi la maofisa waandamizi wa Polisi ambao waliingia kwenye mtego na kutuma fedha, ili watoto wao watafutiwe kazi kwenye idara nyeti za Serikali.
Vyanzo vya kuaminika vililiambia Mwananchi kuwa mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina la David Otieno aliyekuwa akijitambulisha kama Meja Jenerali Mrai, alikamatwa Aprili 4, 2022 eneo la Msamvu mkoani Morogoro.
“Sielewi alikuwa anatumia nini kuwafanya hawa maofisa watume fedha kwa mtu ambaye hawajakutana naye, hawamfahamu kwa sura, wanaongea tu kwa simu na wanajua kuna utapeli mwingi kwa njia ya mtandao,” kilidokeza chanzo kimoja.
“Kuna RPC mmoja alituma fedha kwa awamu mbili za Sh100,000 na Sh50,000 ili mtoto wake atafutiwe kazi katika moja ya idara za Serikali na mwingine akatuma Sh400,000. Yaani ni simulizi ambazo zinachekesha kidogo,” ilielezwa.
Chanzo kingine kilidai “Kuna ofisa mmoja alitaka apandishwe cheo na akatuma Sh270,000 na baadaye akamtumia jamaa zawadi na jamaa akapokea mzigo huo jijini Dar es Salaam.
“Huyo jamaa amekiri kufanya matukio zaidi ya 25 na hayo ni kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, haieleweki kama kuna makundi ya maofisa kutoka idara zingine,” alidokeza ofisa mmoja wa Polisi wa Morogoro aliyekataa kutajwa jina gazetini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alipotafutwa na Mwananchi juzi na jana kuzungumzia suala hilo, alisema hawezi kuzungumzia kwa sababu si la kipolisi na hata kama lingekuwa la kipolisi, lingeweza kuzungumziwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi au Mkuu wa jeshi hilo (IGP), Simon Sirro.
Lakini vyanzo vya uhakika vya Mwananchi kutoka mkoani Morogoro na maeneo mengine vilisisitiza mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 4 na mpaka jana mchana alikuwa bado anashikiliwa na polisi mkoani humo kwa hatua zaidi.
Mwananchi liliendelea kudokezwa na vyanzo vingine kuwa wapo maofisa walijikuta wakiingia kwenye mtego wa mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kuwashawishi kutuma viwango tofauti vya fedha, lakini hawakutuma baada ya kumtilia shaka.
“Maofisa wengine ni kama walikuwa tomaso, wakakubaliana kwamba akifanikisha ama kumhamisha kwenda anakotaka au kuwasaidia ndugu na jamaa zao ndio wangetuma zawadi kama asante. Hiyo ndio pona yao,” kilidokeza chanzo chetu.
Wengine waliahidi kutoa fedha taslimu kati ya Sh500,000 na Sh1,000,000, lakini hawakutuma na baadhi yao ni wale waliotaka kupata wadhifa katika vituo vya kazi ambayo walikuwa wameichagua.
Mwananchi lilipoendelea kuitafiti habari hiyo, lilifanikiwa kupata taarifa kutoka Morogoro zikidai baada ya mtuhumiwa kukamatwa katika nyumba moja ya wageni iliyopo eneo la Msamvu na kupekuliwa, alikutwa na vitu mbalimbali, ikiwamo simu ya upepo (radio call) aina ya Baofeng.
Katika siku za karibuni, kumeibuka makundi ya watu wanaojihusisha na utapeli wakitumia majina ya viongozi na watendaji wenye uamuzi serikalini na kwa sehemu kubwa ya wanaotapeliwa ni wanaotaka vyeo au ajira serikalini.
Kauli ya Polisi
Akizungumzia suala hilo kwa mara nyingine jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Musilimu alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa si la polisi.
“Mimi siwezi kuongea kwa sababu sielewi chochote kuhusu suala hilo, hiyo taarifa hata mimi nimeiona kwenye mitandao tu,” alisema Kamanda Musilimu.
Aliongeza kuwa kama suala hilo lingekuwa la kipolisi, lingeweza kuzungumzwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi au Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.
Jitihada za kumtafuta Sirro zinaendelea kwa kuwa jana hazikuweza kuzaa matunda hata alipopigiwa kwa simu yake ya kiganjani.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime alipoulizwa kuhusu taarifa za kutapeliwa kwa maofisa hao, alijibu kwa njia ya WhatsApp kwa kutuma ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa Twitter wa Jeshi la Polisi ukionyesha kwamba taarifa hiyo ni feki, ipuuzwe.
Alipoulizwa kuwa Mwananchi lina taarifa za kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, ambaye bado anashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi mkoani Morogoro, Misime hakujibu tena swali hilo.
Mtuhumiwa akamatwa
Vyanzo mbalimbali vya habari mkoani Morogoro vinaeleza kuwa ni kweli mtuhumiwa huyo anashikiliwa na polisi mkoani humo.
Chanzo kingine kilisema mtuhumiwa huyo aliwatapeli kwa kuwaambia watu, wakiwemo maofisa wa polisi kuwa anaweza kuwahamisha, kuwapandisha vyeo na wengine kuwatafutia ndugu zao nafasi za kazi kwenye majeshi.
“Ni kweli huyo mtu amekamatwa na hili suala lipo kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Morogoro (RCO), yeye anaweza kulielezea vizuri zaidi kwa kuwa suala hili lipo mezani kwake,” kilisisitiza chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina.