Vita vya Ukraine: 'Wanajeshi wa Urusi walinibaka na kumuua mume wangu'



Warusi wamejiondoa katika maeneo karibu na Kyiv, lakini wameacha watu wakiwa wamejeruhiwa sana ambao hawataweza kamwe kupona kutokana na kiwewe. BBC imesikia ushuhuda wa moja kwa moja na kupata ushahidi wa wanawake wa Ukraine kubakwa na wanajeshi wavamizi.

Onyo: Ripoti hii ina maelezo ya wazi ya unyanyasaji wa kijinsia

Katika eneo tulivu, la mashambani lililo kilomita 70 (maili 45) magharibi mwa Kyiv, tulizungumza na Anna, mwenye umri wa miaka 50. Tumebadilisha jina lake ili kulinda utambulisho wake.

Anna alituambia kwamba tarehe 7 Machi alikuwa nyumbani na mumewe wakati askari wa kigeni alipoingia.

"Akiwa amenielekezea bunduki, alinipeleka kwenye nyumba iliyokuwa karibu. Aliniamuru: 'Vua nguo zako la sivyo nitakupiga risasi.' Aliendelea kunitishia kuniua ikiwa sitafanya kama alivyosema. Kisha akaanza kunibaka," alisema.

Anna alimwelezea mshambuliaji wake kama mpiganaji mchanga, mwembamba wa Chechnya aliyeshirikiana na Urusi.

"Wakati akinibaka, askari wengine wanne waliingia. Nilidhani kwamba imekwisha. Lakini walimchukua mume wangu. Sikumuona tena," alisema. Anaamini aliokolewa na kitengo tofauti cha askari wa Urusi.

Anna alirudi nyumbani na kumkuta mumewe. Alikuwa amepigwa risasi ya tumbo.

"Alijaribu kunikimbilia ili kuniokoa, lakini alipigwa na risasi nyingi," alisema. Wote wawili walitafuta makazi katika nyumba ya jirani. Hawakuweza kumpeleka mumewe hospitali kwa sababu ya mapigano. Alikufa kwa majeraha yake siku mbili baadaye.

Anna hakuacha kulia huku akitusimulia hadithi yake. Alituonyesha mahali ambapo yeye na majirani zake walimzika mume wake nyuma ya nyumba yao. Msalaba mrefu, wa mbao umesimama kwenye kichwa cha kaburi. Anna alituambia kwamba anawasiliana na hospitali ya eneo hilo na anapata msaada wa kisaikolojia.

Kaburi la mume wa Anna
Askari waliomuokoa walikaa nyumbani kwake kwa siku chache. Anasema walimnyooshea bunduki na kumtaka awape vitu vya mumewe.

"Walipoondoka nilikuta dawa za kulevya na Viagra.Walikuwa wamelewa. Wengi wao ni wauaji, vibaka na waporaji. Ni wachache tu wako sawa," alisema.

Njiani kutoka kwenye nyumba ya Anna, tulisikia hadithi nyingine ya kusikitisha.

Mwanamke mmoja anadaiwa kubakwa na kuuawa, na majirani wanasema ilifanywa na mwanaume yule yule aliyembaka Anna, kabla ya kwenda nyumbani kwa Anna.

Mwanamke huyo alikuwa na umri wa miaka 40. Alitolewa nje ya nyumba yake, wanasema majirani, na kushikiliwa katika chumba cha kulala cha nyumba iliyo karibu ambayo wakazi wake walikuwa wamekimbia vita vilipoanza. Chumba kilichopambwa vizuri, chenye Ukuta wa mapambo na kitanda kilicho na ubao wa dhahabu, sasa ni eneo palipofanyika uhalifu. Kuna madoa makubwa ya damu kwenye godoro na duvet.

Katika kona, ni kioo ambacho kimeandikwa juu yake na lipstick - "Kuteswa na watu wasiojulikana, kuzikwa na askari wa Kirusi," inasema.

Kioo ambacho kimeandikwa juu yake na lipstick - "Kuteswa na watu wasiojulikana, kuzikwa na askari wa Kirusi,
Oksana, jirani yake, alituambia kuwa ulikuwa umeachwa hapo na askari wa Urusi ambao walipata mwili wa mwanamke huyo na kumzika. "Wao [askari wa Urusi] waliniambia kuwa alibakwa na kwamba koo lake lilikuwa limekatwa au kuchomwa kisu, na alivuja damu hadi kufa. Walisema kulikuwa na damu nyingi."

Mwanamke huyo alizikwa kwenye kaburi kwenye bustani ya nyumba hiyo.

Siku moja baada ya sisi kumtembelea, polisi waliufukua mwili wake ili kuchunguza kisa hicho. Mwili huo ulipatikana bila nguo, na ukiwa na majeraha makubwa ya kukatwa shingoni.

Andrii Nebytov, mkuu wa polisi wa mkoa wa Kyiv, alituambia kuhusu kesi nyingine wanayoichunguza katika kijiji kilicho kilomita 50 (maili 30) magharibi mwa Kyiv.

Familia ya watu watatu - wanandoa wa miaka thelathini na mtoto wao mdogo - waliishi katika nyumba kwenye ukingo wa kijiji.

"Mnamo tarehe 9 Machi, wanajeshi kadhaa wa jeshi la Urusi waliingia ndani ya nyumba hiyo. Mume alijaribu kumlinda mkewe na mtoto wake. Kwa hiyo wakampiga risasi uwanjani," alisema Bw Nebytov.

"Baada ya hapo askari wawili walimbaka mke mara kwa mara, walikuwa wakitoka na kisha kurudi, walirudi mara tatu kwa ajili ya kumbaka, walitishia kwamba akikaidi watamdhuru mtoto wake mdogo, ili kumlinda mtoto wake hakupinga. "

Askari hao walipoondoka waliteketeza nyumba na kuwapiga risasi mbwa wa familia hiyo.

Nyumba ya familia ikiwa imechomwa moto
Mwanamke huyo alitoroka na mwanawe na kisha kuwasiliana na polisi. Bw Nebytov anasema timu yake imekutana naye na kurekodi ushuhuda wake.

Wamekuwa wakikusanya ushahidi katika nyumba ya familia - ganda lake pekee ndilo limesalia. Ishara chache tu za maisha ya zamani ya amani na ya kawaida yapo kwenye magofu yaliyochomwa. Tuliona baiskeli ya mtoto, mwanasesere wa farasi , kamba ya mbwa na viatu vya manyoya vinavyotumikwa kwenye majira ya baridi.

Mume alizikwa kwenye bustani na majirani. Polisi sasa wameufukua mwili wake kwa uchunguzi. Wanapanga kupeleka kesi katika mahakama za kimataifa.

Afisa anayechunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu wa Ukraine Lyudmyla Denisova anasema wanaandika kesi kadhaa kama hizo.

"Takriban wasichana na wanawake 25 wenye umri wa miaka 14 hadi 24 walibakwa wakati wa uvamizi katika orofa ya nyumba moja huko Bucha. Tisa kati yao ni wajawazito," alisema. "Askari wa Urusi waliwaambia wangewabaka hadi kufikia hatua ambayo hawataki kufanya ngono na mwanaume yeyote, ili kuwazuia kupata watoto wa Ukraine."

mwanasesere wa farasi
Anasema wanapokea simu kadhaa kwenye laini za usaidizi - na pia kupata habari kupitia chaneli kwenye programu ya kutuma ujumbe ya Telegram.

"Mwanamke mwenye umri wa miaka 25 alipiga simu kutuambia dada yake mwenye umri wa miaka 16 alibakwa barabarani mbele yake. Alisema walikuwa wakipiga kelele 'Hii itatokea kwa kila kahaba wa Nazi' walimbaka dada yake," Bi Denisova alisema.

Tuliuliza ikiwa inawezekana kutathmini ukubwa wa uhalifu wa kingono uliofanywa na wanajeshi wa Urusi wakati wa uvamizi huo.

"Haiwezekani kwa sasa kwa sababu si kila mtu yuko tayari kutueleza kilichowapata. Wengi wao kwa sasa wanahitaji usaidizi wa kisaikolojia, kwa hivyo hatuwezi kurekodi uhalifu huo isipokuwa watupe ushuhuda wao," Bi Denisova alisema.

Anasema Ukraine inataka mahakama maalum iundwe na Umoja wa Mataifa kumshtaki Vladimir Putin binafsi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na ubakaji.

"Nataka kumuuliza Putin, kwa nini hii inatokea?" Alisema Anna, mwanamke aliyetuambia alibakwa. "Sielewi. Hatuishi katika Enzi ya Mawe, kwa nini hawezi kujadiliana? Kwa nini anavamia na kuua?"

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad