Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya jana kuwa hali ya serikali ya Ukraine iko hatarini, wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akitoa ombi la kupelekewa kwa ndege zaidi nchini humo huku vikosi vya Urusi vikiendelea kushambulia maeneo ya kimkakati kwa makombora na mizinga.
Putin ameendelea kuwalaumu viongozi wa Ukraine kwa mashambulizi ya Urusi dhidi yake na kuonya kuwa iwapo wataendelea kufanya wanachokifanya, basi wanatilia shaka mustakabali wa serikali ya Ukraine.
Lakini Zelensky amehimiza upinzani, akisema raia wa nchi hiyo wanaendelea kudhibiti miji muhimu ya Kati na Kusini Mashariki mwa Ukraine.
Katika hotuba kwa taifa iliyotolewa kwa njia ya video, alitoa wito kwa raia wa nchi hiyo katika miji iliyotekwa na vikosi vya Urusi kupigana.