Diamond Platnumz.
KAMA ilivyo kawaida, kwenye maisha, kila mtu ana nafasi au zamu yake ya kung’ara na kutaradadi. Ndivyo ilivyo katika maisha ya kila mtu, haijalishi taaluma.
Katika ukanda wa Afrika mashariki, tasnia ya muziki ndiyo inaendelea kukua kila uchao, huku wasanii wapya wakikaribishwa kwenye tasnia hiyo kila siku.
Itakumbukwa tangu enzi za miaka ya 2000, kulikuwa na wasanii wengi, tena wazuri na wenye vipaji vikubwa na sauti tamu za kuimba na walijua kutunga mashairi, lakini wote hao kama ilivyo kawaida walitisha kwa muda wao na kunyauka kama vile maua.
Tasnia ya muziki nchini Tanzania kwa mfano; kulikuwa wasanii wazuri kama Mr Nice, Juma Nature, AY na wengine.
Ni uongo kusema hawakutisha na kuvuka mipaka mpaka kuijenga heshima ya majina yao katika mawimbi ya mataifa jirani.
Lakini pia muda wao wa kuondoka kwenye steji ulipofika walisepa na kuwapisha wasanii wapya kama kina King Kiba, Diamond Platnumz na wengine wengi ambao wameendeleza gurudumu hilo mpaka hivi sasa.
Hawa pia ni binadamu na muda wao bila shaka utafika, sasa mijadala mitandaoni ni kuhusu wale watakaovalia viatu vya wasanii wakubwa kwa mfano Diamond pindi mchezo wake wa usanii utakapomuonesha taa nyekundu.
Baada ya kutathmini kwa muda, wengi wanampigia upatu msanii Harmonize kuliziba pengo litakaloachwa na Diamond wakati atashuka viwango vya muziki mzuri.
Lakini pia licha na Harmonize kupigiwa upato, bado ana kazi kubwa sana ya kuifanya.
Kwa mujibu wa mdau mmoja anayekwenda kwa jina Hope Tyga kwenye Instagram, Harmonize ana mambo mengi tu anayostahili kuyazingatia ili kurithi nafasi ya Diamond kimuziki.
Tyga anaamini ipo siku moja tu ambapo Harmonize atampindua Diamond na umaarufu pamoja na utajiri wake utazidi hata ule wa sasa wa Diamond, ila kuna mambo ambayo yanayomhusu Harmonize kama anapania kupiku rekodi za Diamond.
Kwanza anasema asitegemee huruma ya Watanzania; Harmonize aache kuanika mabaya ya Diamond ili tu Watanzania wamuonee Huruma, afunge domo lake asimuongelee
vibaya Diamond. Hii itamsaidia kupata mashabiki wengi zaidi.
Pia Harmonize anatakiwa akubali kwamba Diamond ana mchango mkubwa kwenye muziki wake.
Hata hivyo, Harmonize anakiri kabisa kwamba bila Diamond yeye asingekuwa hapo. Hii ni nzuri sana na inabidi asisahau kabisa umuhimu wa Diamond, hii pia itamsaidia kupata mashabiki na baraka tele.
Baada ya hapo anapaswa kupunguza kiki za kishamaba. Harmonize au Harmo asiendekeze kiki za kijinga, zinampotezea sana mashabiki. Pia watu wengi wataanza kumpuuza na wamuone kama mtoto vile, afanye kazi, asiendekeze kiki.
Harmonize anapaswa akomae kifikra. Kuna kolabo Harmonize anafanya ambazo hazina faida. Mfano; ile ya Mabantu na Omoyo; yaani alionekana kukurupuka na inabidi aangalie kimataifa zaidi, asiendelee kunga’nga’na hapahapa Tanzania.
Diamond aliamua kabisa kuvuka boda na akafanikiwa kweli hivyo Harmonize afuate nyayo hizohizo.
Yafaa kabisa, Harmonize asiwe kama yule mfalme. Yaani katika vitu muhimu kabisa, isije ikatokea Harmonize akawa na bifu zito na Diamond kama ambavyo King Kiba na Diamond walivyo.
Ikibidi Harmonize amalize bifu kabisa na Diamond, maana Diamond ana mashabiki wengi, ukijenga naye bifu, watu wake kibao watakukataa na hutaendelea kimuziki hivyo Harmonize afanye juu chini bifu lake na Diamond lisiwe kubwa.
Hivi unajua tofauti kubwa kati ya Diamond na Harmonize, hasa katika kipindi hiki ambapo wengi wanajaribu kuwafananisha wawili hao kutoka mafanikio ya kimuziki, maisha, fasheni na utajiri?
Wengi wanajiuliza mbona Diamond ametia fora sana katika kutawala sanaa ya Bongo kimuziki kwa miongo kadhaa bila kufifia kama wenzake walioanza nao, lakini je, wamewahi kujiuliza ni nini kinamfanya Diamond kuzidisha umaarufu wake kutoka kwa vizazi vya jana hadi vizazi vya leo?
Majibu yote haya utayapata katika makala f’lani ambayo imeandikwa na mdau huyo aitwaye Hope Tyga kuhusu ni kwa nini itamgharimu Harmonize muda mwingi wa kujifunza kutoka kwa Diamond ili kumfikia katika ufanisi.
Kwa mujibu wa jamaa huyo, wakati Diamond ameelekea Ulaya katika shughuli rasmi za kimuziki, Harmonize bado yupo nyumbani anazidi kulilia mapenzi na kumfuata mwanamke ambaye hamtaki, nazungumzia Harmonize akizidi kumfuata Kajala Masanja kumrudia kimapenzi.
Tunaona hivi sasa Diamond yupo Bara la Ulaya, hajaenda kwa ajili ya kutalii, ameenda kikazi zaidi, tunaamini safari yake hii italeta faida kubwa katika muziki wake na biashara zake kwa jumla.
Wakati Diamond akipambana ili muziki wake upenye barani Ulaya tunamuona Harmonize akiwa Bongo anapoteza muda tu, yeye kila siku ni kulialia tu, mara aombe msamaha kwa Kajala, ni vituko tu.
Mdau huyo anazidi kumtaka Harmonize kuachana na kukimbizana na wanawake kwani hayo ni mambo ya kupita tu na badala yake kuelekeza muda wake mwingi katika kuipalilia nyota yake kwani asipofanikiwa atasahau kwamba hakutia bidi na kusingizia ulozi.
Hii ni tahadhari ili baadaye asipofanikiwa asilaumu kwamba anarogwa, wakati ukweli unaonesha kabisa kijana siyo mchapakazi, yeye anawaza wanawake tu, hana anachowaza zaidi.
Mwenzake Diamond amelamba ubalozi wa simu, yeye hajapata hata ubalozi wa chaki kwa sababu anajiita Teacher Konde.