LICHA ya kwamba mkataba wake unaelekea ukingoni huku akihusishwa na kurejea Azam, kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula juzi usiku alitamka kauli ambayo ni wazi msimu ujao atakuwa Msimbazi.
Kipa huyo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wakitokea nchini Afrika Kusini walikotolewa na Orlando Pirates alisema; “Tuna kazi kubwa msimu ujao.”
“Binafsi naona tunapiga hatua kuanzia robo fainali ya kwanza mpaka ya tatu kuna maendeleo makubwa, kwa hiyo naona msimu ujao tunaweza tusiishie tulipoishia leo bali tukaanzia hapa,” alisema Manula ambaye habari za chinichini ni Azam walimwekea cheki mezani mwezi mmoja uliopita na wanamsikilizia yeye.
Manula aliongeza akisema; “Naona kabisa tunazidi kukua na robo fainali ya msimu ujao naona tutapata makubwa zaidi ya haya kwa sababu maendeleo yanazidi kuonekana, muendelezo ni mzuri kuliko misimu iliyopita.”
Akizungumzia kuhusu kiwango chake alisema; “Anakua kwa sababu anacheza mechi nyingi, pia ushirikiano mzuri katika kitengo chao cha makipa kwani wanaombeana kwa pamoja hata yeye anapokuwa nje anamombea mwenzake afanye vizuri.”
Kauli hiyo ni kama faraja kwa viongozi na mashabiki wa Simba ambao wengi wao walikuwa wameshaanza kuingia wasiwasi kama kipa huyo anaweza kuondoka baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu.
Kipa huyo akiwa na Simba amechukua makombe ya Ligi Kuu manne na tuzo ya kipa bora wa Ligi mara tatu, pia amecheza robo fainali tatu za Mashindano ya kimataifa Afrika, mbili zikiwa za Ligi ya Mabingwa na moja ya Shirikisho, Ngao mara tatu huku Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mbili.