Wanaomaliza mikataba Yanga wakabidhiwa kwa Nabi
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Dk. Mshindo Msolla, amesema suala la wachezaji wao wanaomaliza mikataba wamemkabidhi Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Akizungumza hivi karibuni, Dk. Msolla amesema awali walishaanza mazungumzo na wachezaji hao kwa ajili ya kutaka kuwapa mikataba mipya, lakini kocha huyo akataka kuachiwa yeye jambo hilo.
"Tuna idadi kubwa ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwezi Agosti, lakini kocha amesema tumkabidhi kazi hiyo, ndiye atakayependekeza mchezaji gani apewe mkataba mpya na nani aachwe," alisema Msolla.
Kiongozi huyo amesema wanaridhishwa na mwenendo wa timu yao, tangu mwanzo wa msimu mpaka sasa na wana matumaini makubwa ya kuwa mabingwa msimu huu.
Amesema ushindi walioupata Jumatano dhidi ya Azam FC umewaongezea imani ya kutamba msimu huu, baada ya kumaliza misimu minne bila taji lolote.
Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 51 katika michezo 19 iliyocheza, huku mabingwa watetezi Simba wakishika nafasi ya pili na pointi 40.