Zaidi ya watu 9,000 wametia saini ombi la mtandaoni la kudai haki kwa niaba ya mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Osinachi Nwachukwu na watu wengine wanaodaiwa kuwa waathiriwa wa unyanyasaji wa nyumbani nchini Nigeria.
Pia wanatoa wito kwa sheria ya kushughulikia unyanyasaji wa nyumbani.
Kifo cha Nwachukwu kimezua ghadhabu miongoni mwa Wanigeria na kuibua mjadala kuhusu ndoa, unyanyasaji wa nyumbani na talaka.
Hapo awali, mwimbaji huyo alisemekana kufariki kwa saratani ya koo, lakini marafiki na familia walidai kwamba alikuwa mwathirika wa unyanyasaji wa nyumbani.
Mume wake, Peter Nwachukwu anazuiliwa na polisi lakini hajashtakiwa kwa kosa lolote. Uchunguzi bado unaendelea.
Waziri wa Masuala ya Wanawake nchini Nigeria Pauline Tallen ameahidi kumtafutia haki Nwachukwu.
Hakuna sheria ya kitaifa dhidi ya unyanyasaji wa nyumbani nchini Nigeria.
Sheria ya Marufuku ya Unyanyasaji dhidi ya Watu iliyopitishwa mwaka wa 2015 inatumika mji mkuu wa Abuja pekee.