Warioba "Nyerere Alikwenda Kanisani Kama Muumini..Hata SIKU Moja Hakutaka Kuzungumza Kanisani"

 


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akienda kanisani kama muumini na sio Rais.


Jaji Warioba ameyasema hayo leo Aprili 23, 2022 katika sherehe za kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere zilizofanyika nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam.


Amesema kuwa mwalimu Nyerere alikuwa anasema anaenda kanisani kama Julius muumini wa dini ya kikatoliki na sio Rais Nyerere.


“Wengi hapa wamesema mwalimu alikuwa mchamungu, alipokuwa hapa kila siku asubuhi lazima aende kanisani pale St. Peter kisha anarudi nyumbani anakunywa chai. Alikwenda kama muumini anapokea neno la Mungu kutoka kwa padri anamuona ni kiongozi wake akimaliza anatoka.


“Yeye mwenyewe alikuwa anasema anayekwenda pale kanisani ni Julius muumini wa dini ya kikatoliki haendi pale Rais Nyerere.


“Akitoka huko atakuja kufanya kazi kama Rais Nyerere, hata siku moja hakutaka kuzungumza kanisani, alikuwa anataka kukwepa kuingiza siasa kwenye nyumba ya ibada,” amesema.


Ameongeza kuwa, mwalimu Nyerere alikuwa muadilifu, muaminifu na mwenye nidhamu kwa nchi yake na ndio maana aliichukia rushwa.


“Wapo hapa ambao tulifanya nae kazi katika lile baraza la mawaziri, Mwalimu ilikuwa kila baada ya muhula atawaambia mawaziri wake mkumbuke cabinet inakutana mara mbili kwa mwezi mpange shughuli zenu mkizingatia kwamba kipaumbele ni cabinet (baraza la mawaziri).


“Cabinet inakutana saa 4:00 asubuhi, Mwenyekiti alikuwa ikifika saa nne kasoro dakika mbili anaingia ndani ya ukumbi, anapanga makaratasi yake ikifika saa nne kazi inaanza kama kuna waziri ambaye hajaingia milango inafungwa na ndivyo ilivyokuwa, hakuna waziri aliyekuwa anachelewa,” amesema

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad