DAKIKA 90 zimemalizika katika Uwanja wa Azam Complex kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Azam.
Azam ilikuwa timu ya kwanza kupata bao kupitia kwa Rodgers Kola dakika ya 11, huku Djuma Shabani akiisawazishia Yanga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 17, kabla ya Fiston Mayele kuiandikia bao la pili na ushindi dakika ya 76.
Bao hilo kwa Mayele anaendelea kushikilia usukani kwenye vita ya ufungaji bora kwani hadi sasa anafikisha mabao 11, akiwaacha Reliants Lusajo (Namungo) mwenye 10 na George Mpole wa Geita Gold mwenye tisa.
Kwa matokeo haya Yanga inaendelea kushikilia rekodi ya kutokufungwa msimu huu ikifikisha pointi 51, baada ya kucheza michezo 19.
Kwa upande wa Azam inaendelea kushikilia nafasi ya tatu na pointi 28, baada ya kucheza michezo 19, huku kikiwa ni kipigo cha pili kutoka kwa Yanga kufuatia mzunguko wa kwanza kufungwa mabao 2-0, Oktoba 30, 2021.