YANGA inaendelea na kambi kumalizana na Azam FC na mzuka mkubwa ukiwa kurejea kwa mastaa wao sita ambao walikaa nje kwa muda mrefu kwa majeruhi.
Yanga imewapokea wachezaji wao mabeki Kibwana Shomari,Abdallah Shaibu ‘Ninja’,David Bryson,washambuliaji Yusuf Athuman na Crispin Ngushi huku Khalid Aucho akiwa sawa ingawa anasubiriwa kujiunga na wenzao akitokea katika kikosi cha timu ya taifa lake la Uganda.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze ambaye alikuwa na vijana hao kambini kwa zaidi ya wiki nzima alisema kurejea kwa wachezaji hao ingawa kiwango chao bado hakijamfurahisha sana kutaleta changamoto ya ushindani.
“Hili la majeruhi lilitusumbua sana hapo nyuma lakini kurejea kwa hawa wachezaji waliocheza leo ni hatua kubwa kwa timu ingawa tumewapa muda wa kucheza kwa dakika 45 lakini kama timu ni morali nyingine kwetu,”alisema Kaze.
“Siwezi kusema nimeridhika na kiwango chao kuna mambo ambayo tunatakiwa kuyaboresha zaidi ili wawe bora na hata timu ilivyocheza kwa ujumla.”
“Tuna ratiba ngumu ya ligi ndani ya Aprili tuna mechi kama tatu utaona hakuna muda ambao ungeweza kupata nafasi ya kuingiza vitu vipya katika muda huo kisha ukapata muda wa kucheza mechi ya kirafiki kupima.
“Sasa tumepata na tumeona haya ambayo tumeyapima tunakwenda kuyatumia kwa ukamilifu katika maandalizi dhidi ya Azam na hata katika mchezo huo na mingine inayokuja.”
Yanga inakutana na Azam Aprili 6, kisha baada ya hapo itarudi Kwa Mkapa kuvaana na Geita Gold katika mchi ya robo fainali ya ASFC kabla ya kukabiliana na watani zao, Simba katika mechi itakayopigwa Aprili 30.