YANGA imejikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 54 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkapa kuanzi saa 1:00 usiku, lakini mapema tu kocha wa wababe hao wa Jangwani, Nasreddine Nabi aliwatumia salamu wapinzani wao, Simba, akiwaambia wamalizane na Orlando Pirates, wao wanawasubiri Kwa Mkapa.
Nabi amewahakikishia mashabiki wa Yanga wasiwe na hofu na kikosi chao ambacho kiliondoka na ushindi kutoka kwa Namungo, akisema licha ya kikosi kufanya makosa ya hapa na pale katika mchezo huo, lakini wako tayari kumalizana na wekundu hao Jumamosi, Aprili 30. Katika mchezo wa juzi Yanga ndio waliouanza kwa kasi dakika ya pili tu, lakini walipoteza nafasi nzuri kupata bao baada ya shuti kali la Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka nje kidogo akipokea pasi ya Fiston Mayele.
Dakika mbili baadaye Fei tena alipoteza nafasi baada ya kuwatoka mabeki wa Namungo kisha kukutana uso kwa uso na kipa David Kissu na kupiga shuti alilopaisha.
Baada ya mashambulizi hayo ya wenyeji, Namungo walizinduka na dakika ya sita walipoteza nafasi nzuri ya kufunga kwa adhabu ndogo iliyopigwa na David Molinga lakini alipaisha iliyotokana na winga Shiza Kichuya kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Yanga walihitaji dakika 17 kupata bao la kuongoza lililofungwa na Mayele akiunasa mpira uliompita beki wa Namungo, Abdul Malick kufuatia pasi ya beki wa yanga, Djuma Shaban kisha akatulia na kumfunga kwa urahisi.
Hilo linakuwa bao lake la 12 akizidi kupaa akiwazidi Reliants Lusajo na George Mpole ambao kila mmoja wamefunga mabao 10.
Yanga waliendelea kutafuta mabao, lakini dakika ya 29 mabeki wa Namungo walifanya kazi ya ziada kumbana Mayele akashindwa kufunga kwa kichwa krosi ya Jesus Moloko. Namungo walirudi mchezoni na kusawazisha bao katika dakika ya 33 kwa bao kali la mbali lililofungwa na Kichuya baada ya mpira kumgusa beki Yannick Bangala. Hata hivyo Yanga walipata bao la ushindi dakika ya 39 kwa bao la Fei Toto akimalizia vizuri pasi ndefu ya Khalid Aucho.
Kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko makubwa kwa upande wa matokeo, ingawa Namungo walirejea na kasi na hasa kadri mchezo ulivyoelekea ukingoni.
Timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa katika vipindi vyote, lakini hadi kipenga cha mwisho Yanga iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 ukiwa ni wa kwanza dhidi ya Namungo tangu ipande Ligi Kuu huku ukiwa ni wa 17 katika mechi 20 za Ligi Kuu msimu huu.
Kocha msaidizi wa Namungo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema washambuliaji wake wangekuwa makini kama alivyo Mayele, basi timu yake ingepata ushindi katika mchezo huo, huku kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze akiwapongeza nyota wake kwa ushindi huo.
Baada ya mchezo wa jana Yanga watapumzika kwa siku mbili kisha wataingia kambini haraka Jumatatu asubuhi kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.
NABI vs SIMBA
Mapema katika mahojiano ya Mwanaspoti, Kocha Nabi alisema hawana kipya sana cha kujiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba kwani maandalizi yalishafanyika katika mechi 20 walizocheza. “Tumekuwa katika ubora katika mechi zote 20 tulizocheza. Tulipoanza msimu tulikuwa na maandalizi bora kwa kila timu tutakayokutana nayo ikiwemo Simba,” alisema Nabi ambaye.
“Ili uwe bingwa hutakiwi kujiandaa kwa akili ya kukutana na Simba pekee, utashinda mechi mbili za Simba na ukapoteza zingine utashuka daraja, tumekuwa tukijiandaa kiubora kushinda dhidi ya timu yoyote tutakayokutana nayo kwenye ligi.
Aidha Nabi alisema Yanga wanaiheshimu Simba hasa mechi hiyo kwa ubora wao na kikosi chake kitaandaliwa kwa ugumu wa mchezo huo ili wazidi kukimbilia kukamilisha malengo yao.
Alisema wanajua kila kitu juu ya ubora wa Simba iliyo chini ya kocha Pablo Franco na anajua wekundu hao watakuja na nguvu ya kutaka kuwazuia katika kasi yao waliyonayo msimu huu.
“Tunajua utakuwa mchezo mgumu, hii ni mechi inayobeba presha ya nchi, tunaiheshimu Simba lakini hata wao wanajua ubora wetu, naamini watakuja na akili ya kutaka kutupunguza kasi yetu ugumu wa mchezo utakuwa hapo.”
Kocha huyo ambaye amechukua tuzo mbili za kocha bora kwa miezi miwili tofauti aliongeza hata kama ikitokea hatokuwepo anamuamini msaidizi wake Cedric Kaze ni kocha aliye na ubora wa kusimamia dakika 90 za mchezo huo kwa kuwa alishafanya kabla.
“Hakuna tatizo katika kukosekana kwangu, kama itakuwa hivyo, nimekwambia maandalizi ya msingi yanakuwa yameshafanyika kitu muhimu ni kusimama pale wakati wa mchezo. Namuamini sana Kaze ni mtu bora.‘’ ambaye anastahili kusimama na kuongoza timu, alishawahi kabla na timu ikashinda.
“Kitu bora zaidi kwetu idadi ya majeruhi imekuwa ikipungua sana na sasa tulibaki na watu wawili tu ambao hawakuwa sawa Saido (Said Ntibazonkiza) na Yacouba (Songne) ambaye bado atakuwa nje kwa muda zaidi lakini Saido naamini anaweza kuimarika.