UONGOZI wa Yanga SC, umefunguka kuwa, unayahitaji makombe yote wanayoshiriki msimu huu ambayo ni Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikiso la Azam Sports (ASFC).
Leo Jumapili, Yanga wanatarajiwa kukipiga dhidi ya Geita katika mchezo wa robo fainali ya ASFC, unaotarajiwa kufanyika Uwanja wa Mkapa, Dar.
Kikosi cha Yanga.
Akizugumza na Spoti Xtra, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said, alisema: “Tunatakiwa kufanya vizuri katika mashindano tunayoshiriki msimu huu, kuna ligi kuu na Kombe la Shirikisho, yote haya tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri, hayo ndiyo malengo yetu.
“Wachezaji wanatakiwa kupambana na wanatakiwa kufahamu ili kuwa mabingwa, basi tunatakiwa kushinda michezo mikubwa, baada ya kuwafunga Azam FC, hivi sasa tunaenda kupambana na Geita Gold, kisha Simba.”
Katika Ligi Kuu Bara, Yanga inaongoza msimamo kwa kukusanya alama 51 baada ya kucheza mechi 19. Bado mechi 11 kumaliza msimu huu.
Yanga imekosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo ambao umekwenda Simba.