Yanga Yaonyesha Ramani ya Ushindi "Tumejiandaa Kuweka Chumvi Kwenye Kidonda"



WAKATI mabosi wa Yanga wakitamba wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya dabi itakayochezwa keshokutwa, beki wa kulia wa timu hiyo, Djuma Shaaban, yuko katika hatihati ya kuukosa mtanange huo kutokana na kuwa majeruhi.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wachezaji wa timu hiyo wako kamili kuwavaa Simba na kila mmoja anatamani kukutana na wapinzani hao.

Bumbuli alisema benchi la ufundi la timu hiyo linaendelea kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi zilizopita na pia kukiimarisha zaidi kikosi chao kwa sababu wanahitaji matokeo ya ushindi tu na si vinginevyo.

"Timu inaendelea na mazoezi yake kwa ajili ya mchezo wetu huo tukiwa na matumaini ya kupata pointi tatu, kila mchezaji ana kiu na ari ya kuona tunapata ushindi," alisema Bumbuli.

Ofisa huyo amewaomba mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwashangilia wachezaji wao ambao wameahidi kupambana na hatimaye kufikia malengo.


Alisema wamejipanga kushinda mechi hiyo dhidi ya wapinzani wao ambao watakuwa wamerejea nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya kutolewa katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Alitamba Yanga imejiandaa kikamilifu 'kutia chumvi' katika kidonda cha Simba ambayo ilitolewa katika michuano hiyo ya kimataifa kwa penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.

"Mazoezi yanakwenda vizuri, timu iko kambini Kigamboni, tuna majeruhi mmoja tu ambaye ni Djuma Shabaan aliyeumia kwenye mechi iliyopita dhidi ya Namungo, mpaka sasa yupo chini ya uangalizi wa madaktari na tutaangalia nini watasema kuhusiana na afya yake, kama majeraha yake ni makubwa, au ya kawaida tu na anaweza kucheza, " alisema Bumbuli.

Aliongeza licha ya kujipanga, wamejiandaa kukutana na upinzani kutoka kwa Simba kwa sababu hawatakubali kupoteza mchezo huo kirahisi.

"Tunawakaribisha kwenye ligi ambako kuna wafalme wake ambao ni sisi, watakuwa na kazi kubwa ya kuwatuliza mashabiki wao kwa sababu hawana kitu chochote kwa sasa. Utakuwa mchezo mzuri sana, watakuwa wamejiandaa vya kutosha kwa hiyo tunatakiwa tutoe burudani tucheze mchezo mzuri watu wafurahi. Lakini sisi tutakuwa tunacheza tukiwa na amani kwani tunaongoza kwa tofauti ya pointi nyingi, tupo kileleni na hatujapoteza, na tuko kwenye njia nzuri ya kuutwaa ubingwa, kwa hiyo hata tukipoteza mechi moja au mbili, hatuna wasiwasi sana wa kuupoteza ubingwa kutokana na pengo kubwa la pointi liloliweka," Bumbuli alisema.

Simba mabingwa watetezi wa ligi hiyo watashuka dimbani wakiwa na mchezo mmoja pungufu wakati watani zao, Yanga wenye pointi 54 ndio vinara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad