Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaonya watu wake mapema leo kuwa wanajeshi wa Urusi wanaoondoka katika maeneo yao wanatengeneza kile amesema ni "mazingira ya maafa" nje ya mji mkuu kwa kutega mabomu ya ardhini katika eneo zima hata karibu na nyumba za watu na maiti.
Ametoa onyo hilo wakati mzozo wa kiutu katika mji uliozingirwa wa Mariupol ukitokota. Wanajeshi wa Urusi walizuia operesheni za kuwahamisha watu kwa siku ya pili mfululizo hapo jana. Shirika la Msalaba Mwekundu limesema litajaribu tena asubuhi hii kuingia katika mji huo.
Wakati huo huo, Moscow imewatuhumu Waukraine kwa kufanya shambulizi la kutumia helikopta kwenye ghala la mafuta katika ardhi ya Urusi.
Ukraine imekanusha kuhusika na mripuko huo, uliotokea katika mji wa Belgorod. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema shambulizi hilo haliweki mazingira mazuri ya kuendelea kwa mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi.