KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amemaliza muda wake wa uongozi kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na sasa kinachukuliwa na Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana.
Mkongwe huyo wa siasa za Tanzania anachukua nafasi hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kumchagua kwa kura zote kushika wadhifa wake huo mpya ndani ya chama hicho tawala Aprili Mosi, mwaka huu jijini Dodoma.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na kujiuzulu kwa Phillip Mangula, huku chama hicho kikitumia nafasi hiyo kutangaza kuwasamehe baadhi ya makada waliokuwa wamefutiwa uanachama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa TCD, Bernadetha Kafuko, Zitto atakabidhi rasmi kiti kwa Kinana keshokutwa.
Alisema TCD inawajulisha wanachama wake wote, wanachama washiriki (Associate Members), wadau wanaofanikisha kukamilika kwa Mkutano wa Haki, Amani na Maridhiano na wadau wengine wote wa demokrasia nchini kwamba maandalizi ya mkutano yanaendelea vizuri na kuwa mkutano unatarajiwa kufanyika tarehe 5 na 6 Aprili, mwaka huu kama kilivyoeleza awali katika taarifa zake.
Alisema kituo kinawahakikishia wadau wote na wananchi kwa ujumla kwamba ushirikiano ambao umekuwa ukitolewa na wadau wanaowezesha kufanyika kwa mkutano huo umekuwa wa kutia moyo na ni imani yao kwamba washiriki wote ambao wamekwishapewa taarifa ya kuhudhuria mkutano ambao utafanyika jijini Dodoma, hivi sasa watakuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuhudhuria mkutano huo muhimu ambao utatoa dira ya uimarikaji wa demokrasia nchini.
"Kituo kinatoa wito kwa wadau na vyama vya siasa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuhakikisha kila mdau anasaidia kukamilika kwa mkutano huo ambao mafanikio yake yataleta tija siyo tu kwa wanachama wa kituo bali pia serikali na nchi kwa ujumla wake.
"Jambo ambalo tungependa kuwahakikishia ni kwamba tumepata imani kubwa kuona namna gani wadau mbalimbali na hasa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini, wamekuwa na hamu kubwa ya kushiriki mkutano huu pamoja na ushawishi wao kwa taasisi mbalimbali za kimataifa katika kuunga mkono juhudi za kituo ili kufanikisha gharama za mkutano.
“Maandalizi yake yapo katika hatua za mwisho ambapo Kamati ya Ufundi ya TCD imekuwa bega kwa bega na watendaji wa kituo katika kukamilisha maandalizi yanayoendelea hivi sasa hapa Dodoma," alisema.
Alisema mkutano huu pia utashuhudia makabidhiano ya uongozi kutoka Chama cha ACT-Wazalendo kama Mwenyekiti wa sasa kwenda kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama mwenyekiti mpya wa kituo.
"Hivyo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, atamaliza muda wake wa uongozi na kumkabidhi mwenyekiti mpya ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana, mnamo Aprili 6, mwaka 2022.”