ASKOFU wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) Jimbo la Ziwa Tanganyika, Charles Katale amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa na Askofu Kiongozi wa KMT, Conrad Sikombe, ilisema Askofu Katale alifariki ghafla Mei 2, mwaka huu, baada ya kuugua muda mfupi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Askofu Katale alifariki dunia wakati uongozi wa jimbo lenye makao makuu Kigoma, ukiwa katika mipango ya kumsafirisha kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa matibabu.
Kiongozi huyo amefariki dunia akiwa ametumikia wadhifa huo na kuwa askofu wa kwanza wa jimbo hilo, kwa takriban mwaka mmoja na miezi minne tangu alipoingizwa kazini Januari 10, mwaka jana, Urambo mkoani Tabora.
Kabla ya kuchaguliwa na kusimikwa katika wadhifa huo, Askofu Katale alikuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Ziwa Tanganyika kwa miaka kadhaa.
“Kutokana na msiba huu, tuendelee kuiombea familia yake, kanisa na jimbo alilokuwa akiliongoza,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, Askofu Kiongozi Sikombe katika taarifa hiyo, alisema Askofu Katale atakumbukwa kama mtu jasiri, mfundishaji mzuri na mhubiri wa injili mwenye karama.
Kuhusu mazishi ya askofu huyo, Katibu Mkuu wa KMT, Mchungaji David Mgombele, alisema maandalizi bado yanaendelea huku akibainisha kuwa viongozi wa kanisa hilo kutoka majimbo mbalimbali wako safarini kwenda Kigoma.
Hata hivyo, alisema ratiba ya awali inaonyesha kwamba mwili wa Askofu Katale utaagwa kesho na kuzikwa Jumamosi mjini Kigoma.