Dar es Salaam. Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) na kampuni ya Marekani ya kutengeneza ndege ya Boeing wameingia mkataba wa makubaliano ya kushirikiana katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili kuleta tija zaidi katika biashara.
Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kubwa ya kimataifa ya utengenezaji wa ndege kuingia mkataba wa namna hiyo na mteja wake.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo murugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema mafunzo yatakayoanza hivi karibuni yatawalenga mameneja wakuu, mameneja wa kati na wasimamizi.
"Tuna bahati ya kuwa na ushirika huu Boeing kuhusu kujenga uwezo. Hili ni jambo la kufurahisha sana na ni wakati muafaka kwa mpango wa kufufua Air Tanzania,” amesema Matindi akielezea shukrani zake.
Juhudi za kufufua ATCL zilianza tangu mwaka 2015 wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Rais John Magufuli, hadi sasa Serikali imenunua ndege tisa zikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner mbili.
"Kwa kufufua shirika letu tulianza na kuleta mameneja wapya vijana wenye nguvu na moja ya masuala ambayo tumekuwa tukipambana nayo ni kuwajengea uwezo," amesema Matindi ambaye anasimamia shirika hilo tangu lilipoanza kufufuliwa.
"Wana uzoefu wakutosha katika uongozi lakini bado ni muhimu kuwaimarisha zaidi katika tasnia ya bviashara ya usafiri wa anga, Tunashukuru ukweli kwamba ninyi (Boeing) mmeamua sio tu kuzingatia kuwafanya ng'ombe wenu wawe wazito lakini kuhakikisha kwamba uzito una athari chanya kwetu kwetu pia," amesema.
Mkurugenzi wa mauzo wa Boeing Mashariki ya Kati na Afrika, Moore Ibekwe amesema hatua yao ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ATCL ni zawadi ya imani ya shirika hilo kwa Boeing.
Tayari ATCL inamiliki ndege mbili aina ya Boieng 787-8 Dreamliner na shirika hilo mwakani litapokea ndege nyingine nne za Boeing ambazo ni Boeing 737-900 Max mbili, Boeing 787-8 Dreamliner moja na Boeing 767 Freighter kwa ajili ya kubeba mizigo.