Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amewaongezea program ya mazoezi wachezaji wake wakiongozwa na Khalid Aucho na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Yanga juzi Jumanne ilielekea Shinyanga kuendelea na kambi ya maandalizi ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Simba utakaochezwa CCM Kirumba, Mwanza, Jumamosi hii.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo anafanya program mbili kwa siku, yaani asubuhi na jioni.
Mtoa taarifa huyo alisema, lengo la kuwaongezea program hizo mastaa hao ni kuwaongezea fitinesi itakayowawezesha kucheza kwa dakika 120.
Aliongeza kuwa, awali kocha huyo alikuwa akiwafanyisha program moja wachezaji wake asubuhi pekee na jioni kutoa muda wa mapumziko.
“Kocha anataka kuona timu yake ikicheza zaidi ya dakika 90 kutokana na ushindani atakaoukuta katika hatua ya nusu fainali.
“Hivyo ameona aongeze program ya mazoezi kutoka mara moja kwa siku asubuhi na kuwa mara mbili na jioni.
“Tangu timu ilivyorejea Shinyanga ikitokea Mwanza ilipokwenda kucheza mchezo wa ligi dhidi ya Biashara, imeendelea na program hizo kwa siku mara mbili,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amezungumzia kambi ya timu hiyo, kwa kusema: “Maandalizi ya timu yetu yanakwenda vizuri, wachezaji wana morali kubwa ya kupata ushindi. Vitu vingine vinavyoendelea ni siri ya kambini.”
STORI; WILBERT MOLANDI