Bagonza Aibuka Sakata kina Halima Mdee "Uamuzi wa Chama Upewe Heshima"



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimeshaandaa barua ya kumpelekea Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, kuhusu uamuzi uliochukuliwa na kamati kuu ya chama hicho wa kuwavua uanachama waliokuwa wanachama wao 19,...

...akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Halima Mdee.

Wakati chama hicho kikiendelea na mchakato huo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, amesema uamuzi uliofanywa na chama hicho unapaswa kupewa heshima huku akiitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bunge, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, serikali na vyama vya siasa kujifunza kutokana na sakata hilo.

Uamuzi wa kuwavua uanachama ulikuja baada ya kwenda kuapishwa na kuwa wabunge wa viti maalumu bila kupata baraka ya chama hicho jambo lililotafsiriwa kama usaliti. Usiku wa kuamkia jana, Baraza Kuu la chama hicho lilibariki uamuzi wa kuwafuta uanachama.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema barua hiyo ipo njiani na muda wowote kuanzia sasa itafika mezani kwa Spika wa Bunge.


HATIMA RUZUKU

Kuhusu ruzuku, Mnyika alisema hawezi kulizungumzia kwa sasa kwa sababu kamati kuu ya chama ndiyo yenye wajibu wa kukaa kikao na kujadili kama watachukua ruzuku au la.

“Kikao cha kamati kuu kina wajibu wa kujadili suala la ruzuku na mpaka sasa bado hawajakaa kikao, kwa hiyo siwezi kulizungumzia mpaka pale kamati hiyo itakapokaa,” alisema.

CHADEMA kilitangaza kususia ruzuku na vyote vinavyopatikana kupitia uchaguzi mkuu uliopita, ikiwamo ubunge wa viti maalum na kueleza kuwa hakitambui matokeo ya uchaguzi huo na mchakato wake.

Kufuatia msimamo huo, CHADEMA iligoma kupeleka kwa msajili wa vyama, jina la akaunti ya Baraza la Wadhamini, ili kuingiziwa fedha za ruzuku.

BAGONZA NA FUNZO

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia uamuzi wa Baraza Kuu CHADEMA, alisema uheshimiwe kama ambavyo wabunge hao walivyokuwa na imani nao kuwa watawatendea haki.

“Wale wabunge 19 nafikiri walikuwa na imani na baraza kuu na ndiyo maana wakaandika rufani yao, huwezi kutuma rufani kwa mtu usiyeamini kuwa atakutendea haki. Kwa hiyo, waliandika rufani zao, baraza limeitisha, limefanya uamuzi, nadhani uamuzi wa baraza uheshimiwe na wote," alisema.

Askofu Bagonza pia alisema kuwa kuna kitu cha kujifunza kama taifa kupitia sakata hilo huku, swali kuu likiwa ni 'kitu gani kiliwapeleka wabunge hao bungeni ilhali chama chao hakikuridhia?'


"Liwe fundisho kwa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama, uongozi wa Bunge wenyewe, serikali, vyama vya siasa, kila mtu ana la kujifunza katika hili," alisema.

Alisema kufuatia uamuzi huo CHADEMA imeonyesha ukomavu wa kisiasa kwa sababu imefanya jambo ambalo vyama vingine vya kisiasa havikufanya, ikiwamo kushirikisha wadau wa siasa katika mchakato wa kufanya uamuzi huo.

“Wamefanya kitu ambacho hakikufanywa na wengi, tumesikia vyama vikifukuza wanachama wake ikiwamo chama tawala (CCM), hatujawahi kusikia mpaka na msajili anashiriki kwenye baraza anaona jinsi mambo yalivyokwenda, naweza kusema wamekomaa,” alisema.

Akiongelea suala la katiba mpya askofu huyo alisema kuwa wakati wa kupata katiba hiyo ulishafika na kupita tangu zamani hivyo kinachohitajika ni mchakato wa upatikanaji wake.

Mchambuzi wa siasa nchini, Gwandumi Mwakatobe, alisema anawapongeza CHADEMA kwa kufanikisha mkutano huo wakiwa wanapitia vikwazo vingi, ikiwamo vya kiuchumi na kisiasa, hasa Mwenyekiti wao Freeman Mbowe na wanachama wengine kuwekwa rumande kwa takriban miezi minane na watu kuingia bungeni bila ridhaa ya chama.

Alisema suala la kina Mdee na wenzake 18 kuvuliwa uanachama siyo jambo geni kwa kuwa walishafukuzwa mwanzo, wakakata rufani lakini uamuzi wa rufani umechukua muda mrefu kutolewa.

Alisema uamuzi huo wa CHADEMA unapaswa kupongezwa kwa uamuzi huo kwa kuwa ulifanywa kwa kufuata demokrasia ikiwamo kufanyika vikao rasmi vya chama.

Alisema uamuzi huo ambao haukufanywa na kiongozi bali wanachama kwa vikao rasmi vya chama unapaswa uigwe na vyama vingine.

"Hao wapongezwe na ndivyo vyama vingine viige, hata CCM waige, wasimsikilize mkuu fulani hamtaki fulani ndiyo anaondoka, hapana! Wanachama wawe na uhuru wa kuamua kipi kifanyike, iwe ni kufukuza au kuingiza," alisema.


Mwandumi pia alisema suala la kudai Katiba Mpya ni muhimu kwa sababu limechelewa kushughulikiwa.

“Tukumbuke kwamba hata Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, alisema katiba hii haifai, akipewa dikteta ni hatari, katiba hii ni ya mwaka 1977 ilitungwa ndani ya chama kimoja, watu wa chama kimoja. Pia ilipofika mwa 1992 hatukupata katiba mpya ila kiliingizwa kipengele cha mfumo wa vyama vingi,” alisema.

MDEE, MBOWE

Aliyekuwa mwanachama wa Chadema, Halima Mdee, alidai hakukuwa na uhuru wakati wa mkutano wa juzi hasa katika upigaji wa kura, akisisitiza kuwa kilichofanyika ni uhuni.

"Huwa nakwepa kuzungumza maneno makali kwa sababu naheshimu viongozi wangu, lakini sikujua kama CHADEMA kunaweza kufanyika uhuni kwa kiwango hiko. Nitaendelea kuwa CHADEMA vizuri tu, lakini kichofanyika pale ni uhuni wa kiwango cha hatari, hata Mbowe mwenyewe anajua," alisema Mdee.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliijibu kauli hiyo kuhusu uamuzi uliofanywa usiku wa kuamkia jana na Baraza Kuu la chama hicho, waliouita wa kihuni, akiwataka na wao kuacha uhuni.

"Wajumbe wamekuja leo na wamefanya uamuzi wakishuhudia na kura zimepigwa mbele yao, waache mambo ya ‘kihuni'," Mbowe alijibu.

Mbali na Mdee, wengine waliovuliwa uanachama ni Grace Tendega, Ester Bulaya, Agnesta Lambert, Jesca Kishoa, Ester Matiko, Salome Makamba na Nusrat Hanje.

Pia wamo Tunza Malapo, Conchestar Rwamlaza, Naghenjwa Kaboyoka, Hawa Mwaifunga, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Asia Mohammed, Sophia Mwakagenda, Cecilia Pareso, Kunti Majala na Felister Njau.

Katika upigaji wa kura, jumla ya wajumbe 423 walishiriki. Kati yao 413 (asilimia 97.6) walikubaliana na uamuzi wa kamati kuu kuwavua uanachama, watano (asilimia 1.2) hawakukubalina na uamuzi wa kuwafukuza huku wasiofungamana na upande wowote wakiwa watano (asilimia 1.2).

VITI VYEUPE BUNGENI

Kwa siku mbili juzi na jana, upande waliokuwa wanakaa wabunge wa viti maalum (CHADEMA) bungeni hawakuwapo, huku Mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia chama hicho, Aida Khenani, akionekana peke yake.

Hata hivyo, Nipashe lilimtafuta Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi ili kufahamu endapo Bunge limeshapokea barua kutoka CHADEMA inayoeleza kuwavua uanachama wabunge hao, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kutokana na kutompata kiongozi huyo kwa njia ya simu, pia kwenda ofisini kwake.

Kuvuliwa uanachama kwa wabunge hao kukiridhiwa na Bunge, kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge zinapaswa kuongozwa na wabunge wa upinzani.

PAC ilikuwa ikiongozwa na Naghenjwa Kaboyoka wakati LAAC ilikuwa ikiongozwa na Grace Tendega.

*Imeandikwa na Jenifer Gilla (DAR) na Augusta Njoji (DODOMA).



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad