Wahamiaji watatu wamethibitishwa kufariki na wengine kumi hawajulikani walipo, huku 40 kati yao wakiokolewa baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Pwani ya Mashariki ya Kati, Tunisia.
Boti hiyo iliyoondoka Pwani ya Sfax ikiwa na zaidi ya wahamiaji 50 raia wa Tunisia, ilizama katika Mji wa Bandari katika jaribio la wahamiaji hao la kuingia Ulaya kinyime na sheria.
Msemaji wa Walinzi wa Kitaifa wa Tunisia, Houcem Jebabli amesema Mji wa Sfax ni mojawapo ya sehemu kuu za kuondoka kwa wahamiaji wa Tunisia na wa kigeni kutoka maeneo mengi ya Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara kuelekea Pwani ya Italia.
“Na kasi ya kuondoka kinyume cha sheria huenda ikaongezeka msimu wa kiangazi unapokaribia maana majira haya hutumika sana na wahamiaji haramu,” amefafanua Jebabli.
Mwanzoni mwa Mei 2022, Serikali nchini Tunisia ilitangaza kupatikana kwa miili 24 ya wahamiaji baada ya boti zao kuzama kwenye ufuo huo wa Sfax.
Vilevile, kati ya tarehe 22 na 30 Aprili 2022, boti nne zilizama katika ufuo wa Sfax na kusababisha kuzama kwa wahamiaji 97 ambao waliokolewa, kupatiwa matibabu na kupona siku zilizofuata.
Mwaka huohuo, wahamiaji wengine 15,671 wakiwemo wanawake 584 walifanikiwa kufika ardhi ya Italia kutoka Pwani ya Tunisia ikilinganishwa na wale 12,883 kati yao wanawake wakiwa 353 kwa mwaka 2020.
“Kiujumla zaidi ya wahamiaji 123,000 walitua Italia mwaka 2021 ikilinganishwa na wahamiaji 95,000 kwa mwaka 2020 ameongeza Jebabli.
Italia ni moja wapo ya sehemu kuu za kuingia Ulaya kwa wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini ambao wanawasili hasa kutoka Tunisia na Libya, nchi mbili ambazo zinaongoza kwa kiasi kikubwa cha wananchi wake kuikimbia tangu mwaka 2021