BRELA kufuta kampuni 5,600



WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetangaza kusudio la kuanza kuzifutia usajili jumla ya kampuni za kibiashara 5,676 zilizoshindwa kukidhi vigezo vya kisheria.

Kwa mujibu wa wakala huo, uamuzi huo unachukuliwa kwa kuzingatia takwa la kisheria la kampuni kuwasilisha taarifa za mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa nchini au mizania ya mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 15.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari, akisema ufutaji wa usajili wa kampuni hizo utafanyika kwa awamu.

Alisema awamu ya kwanza itajumuisha kampuni 5,676. Kati yake, kampuni 5,284 zimesajiliwa nchini na zingine 392 ni zilizosajiliwa nchi za nje na kupata hati ya utambuzi.

Nyaisa alisema hatua hiyo ni kwa mujibu wa vifungu vya 400 na 441 vya sheria ya kampuni ambayo inampa mamlaka msajili wa kampuni kufuta kampuni ambayo haijaonyesha kuendelea kufanya biashara au kuendelea kushikilia majina kinyume cha sheria.


 
“Hali hii inawazuia watu wengi wenye uhitaji wa majina hayo kuyatumia lakini pia inapunuguza Pato la Taifa na kuisababishi hasara kwa serikali.

"Faida ya zoezi ni kuhakikisha daftari la usajili wa kampuni linakuwa na taarifa sahihi za kampuni, daftari kubaki na kampuni ambazo ni hai, kuutaarifa umma kuhusu uhai wa kampuni na kuwakumbusha wamiliki wa kampuni juu la kujumu lao la kuwasilisha taarifa kwa msajili kila mwaka," alifafanua.

Alikumbusha kuwa kifungu cha 128 cha Sheria ya Kampuni, Sura 212, kinazitaka kampuni zilizosajiliwa nchini kuwasilisha taarifa za mwaka, akifafanua kuwa kutowasilisha taarifa hizo kunatoa tafsiri kuwa kampuni hizo hazifanyi biashara kulingana na lengo la kuanzishwa kwake.


Alisema kifungu cha 438 cha sheria hiyo kinazitaza kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi ambazo zinafanya biashara nchini, kuwasilisha mizania ya mwaka, kinyume cha hapo inatafsiriwa kuwa kampuni hizo hazina tawi nchini.

Nyaisa alitoa rai kwa kampuni zilizosajiliwa chini ya sheria hiyo kutekeleza matakwa ya sheria kwa kuwasilisha taarifa za mwaka (Annual Returns) ili kuepuka kufutwa kwenye datfari la kampuni kwa kuwa ufutaji wa kampuni zenye dosari tajwa hapo juu, ni endelevu.

"Kutokana na vifungu tajwa hapo juu, msajili wa kampuni anatoa notisi ya siku 30 kuanzia Mei 30, mwaka huu ili kampuni tajwa zithibitishe kwamba bado zinafanya biashara. Kampuni ambazo hazitatekeleza matakwa ya taarifa hii zitaondolewa katika daftari la kampuni zilizosajiliwa nchini," alionya na kubanisha kuwa orodha kamili ya kampuni hizo inapatikana kwenye tovuti rasmi ya BRELA.

Nyaisa aliendelea kufafanua, akisema: "Endapo kampuni husika, wanahisa au wadeni wa kampuni, zikiwamo taasisi za kifedha na watumishi wa kampuni wanaamini kwamba kampuni iliyoko kwenye orodha hii inafanya biashara na kwamba inapaswa kubaki kwenye daftari la kampuni zote, watoe taarifa kwa msajili wa kampuni kupitia anwani ya Posta."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad