CCM Wajibu Mapigo ya NCCR Mageuzi "Selasini ni Anajitafutia Umaarufu kwa Kuipaka Matope CCM"



KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amesema ajenda kubwa kwa sasa ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhuisha demokrasia nchini.

Alisema hayo kupitia taarifa aliyotoa jana akikanusha madai yaliyotolewa na mwanasiasa Joseph Selasini kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewahi kumtumia James Mbatia au kuwa na ushirikiano na NCCR-Mageuzi.

Alisema CCM inalo jukumu moja la kumuunga mkono Rais Samia katika safari ya maridhiano aliyoianzisha hivyo haiwezi kurudi nyuma.

“Kwa wakati huu CCM kama chama kiongozi na mlezi wa siasa nchini tunalo jukumu moja tu, la kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika safari ya maridhiano aliyoianzisha hivyo hatuwezi kurudi nyuma bali kusonga mbele," alisema.


Shaka alieleza chama kilivyosikitishwa na madai hayo aliyosema ni upotoshaji unaotaka kuihusisha CCM katika sakata linalotoka ndani ya NCCR-Mageuzi.

Alisema kinachofanywa na Selasini ni kujitafutia umaarufu kwa kuipaka matope CCM. “Hivyo kudai aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Dk John Magufuli alikuwa na uhusiano na chama chao ni mambo ya kupuuzwa kwani CCM ni chama kikubwa na taasisi imara ya kisiasa nchini kinachojitegemea katika uendeshaji wa siasa zake na masuala yake.”

Alisema chama hakijawahi kumrubuni mwanasiasa yeyote kujiunga nacho na kwamba wote waliowahi kujiunga, walifanya kwa ridhaa na utashi kujiunga na CCM aliyoiita kuwa ni tanuri la kuoka na kulea wanasiasa.


Alimshauri Selasini na wanasiasa aina yake kujipanga kimkakati kuimarisha vyama vyao ikiwemo kuboresha na kuziishi katiba zao ili kuondokana na migogoro ya madaraka inayozorotesha demokrasia ndani ya vyama vyao.

Hivi karibuni, Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi iliwasimamisha kujihusisha na shughuli zozote ndani ya chama mwenyekiti, Mbatia na sekretarieti yake hatua iliyopingwa na Mbatia
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad