Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimefafanua hatua walizozipitia hadi kufikia uamuzi wa kuwavua uanachama wabunge 19 wa viti maalum (CHADEMA), huku wakisisitiza kuwa hawataingilia taratibu zinazoendelea Mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Benson Kigaila ameeleza kuwa wao hawakuwahi kumteua mtu kuwa mbunge wa viti maalum huku akisisitiza kuwa mpaka sasa hawautambui uchaguzi wa mwaka 2020 wala matunda yoyote ya uchaguzi huo.
Akizuingumzia mchakato wa upigaji kura katika mkutano wa Baraza Kuu wakati wa kuidhinisha kuwafuta uanachama wabunge hao amesema mchakato huo ulikuwa wa wazi.
“Asilimia 97% ya kura za wazi zilizopigwa zilikubali wabunge hao wavuliwe uanachama, huku wajumbe watano walipiga kura ya hapana na wengine watano hawakupiga kura ya kukubaliana na uamuzi wa kuwavua uanachama wakina Mdee” – Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Benson Kigaila