KIUNGO fundi wa Simba, Clatous Chama hataonekana kwenye mechi wala mazoezini kwa mwezi mmoja kutokana na majeruhi yake, Mwanaspoti limejiridhisha.
Staa huyo kipenzi cha mashabiki aliyekuwa analipwa mshahara wa Sh50Milioni akiwa Berkane, hakucheza dhidi ya Namungo kule Ilulu Lindi pamoja na Ruvu Shooting juzi Jumapili Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuibua minong’ono kwamba hana maelewano mazuri na kocha wa Simba, Pablo Franco tangu mechi ya Yanga ilipomalizika kwa matokeo ya suluhu.
Mwanaspoti linafahamu Chama aliyesajiliwa kwa Sh700Milioni kule Berkane, ni majeruhi ya mguu wa kulia chini kwenye maungio ya ugoko na eneo la kukanyagia (Enka),iliyokuwa ikimsumbua tangu alipokuwa anacheza Berkane ya Morocco.
Kwenye mechi ya Yanga licha ya kutokuwa fiti na kushindwa kucheza vizuri Chama alitonesha majeraha yake hayo na kushindwa kusafiri na kikosi kwenda Lindi kwa ajili ya mchezo na Namungo uliomalizika kwa suluhu.
Baada ya majeraha hayo kuendelea kumsumbua, Chama pamoja na vipimo alivyofanya iligundulika anatakiwa kupata muda wa kupumzika nje ya uwanja bila ya kufanya mazoezi yoyote ya kucheza mpira kwa muda usiopungua mwezi mmoja.
Katika kipindi hicho, Chama hataonekana kwenye uwanja wa mazoezi Mo Simba Arena, kusafiri na timu katika michezo ya ugenini wala kwenye mechi yoyote.
Katika kipindi cha mwezi mmoja amekosa mechi mbili dhidi ya Namungo na Ruvu Shooting na hatakuwepo katika michezo mingine minne dhidi ya Kagera Sugar, Azam, Geita Gold, KMC.Lakini vilevile hatacheza dhidi ya Pamba Mei 14 kwenye robo fainali ya ASFC, ila wakifuzu kucheza na Yanga atakuwepo. Kama atapona kwa wakati atarejea Uwanjani Juni 16 dhidi ya Mbeya City na atazikuta mechi dhidi ya Prisons, Mtibwa Sugar na Mbeya Kwanza.
Chama mwenyewe alipoulizwa na Mwanaspoti jana alisema; “Hakuna shida nyingine yoyote kwenye timu inayonifanya kuwa nje zaidi ya haya majeraha,” alisema Chama na kuongeza;
“Sipo katika uwanja wa mazoezi wala mechi kutokana na shida hii ila benchi la ufundi, wachezaji wenzangu na viongozi wanafahamu naendelea na programu maalumu ya mazoezi ya Gym,”
“Mazoezi ya gym nafanya ndani ya kambi yetu kwa maana hiyo naona na makocha na wachezaji wenzangu kama kawaida,”aliongeza staa huyo. Katika programu hiyo maalumu ya mazoezi anayofanya Chama ya gym yupo Chriss Mugalu ambaye ni majeruhi pia.
Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema Chama alipewa muda wa kupumzika kutokana na kuumia katika mechi dhidi ya Yanga.