Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ikitarajia kufanya mabadiliko ya nauli kwa mabasi yaendeyo haraka maarufu mwendokasi, Wakala wa mabasi hayo (Dart) amependekeza kwa njia jumuishi abiria kutozwa Sh1500 kutoka 800 wanayotozwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na kusainiwa na Mkurugenzi wa Latra, Gilliard Ngewe ilieleza wameitisha mkutano wa wadau kutoa maoni ya nauli ya mabasi hayo baada ya kupokea maombi ya kurejea nauli za mabasi hayo kwa mkoa wa Dar es Salaam kutoka Kampuni ya Dart.
Mapitio ya viwango ni kwa mujibu wa kifungu cha 21 cha sheria sura ya 143 mamlaka hiyo inapaswa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi kuhusu viwango vipya vya nauli vilivyopendekezwa.
Katika mapendekezo yao, Dart wanataka njia kuu ambazo abiria wanatozwa Sh650 kwa sasa wamependekeza ipandishwe hadi Sh1,200 na kwa njia mlishi walizokuwa wanatozwa Sh400 Sasa wamependekeza Sh600.
Kwa upande wa njia jumuishi wanazotoza nauli ya Sh800, Dart wamependekeza abiria watozwe Sh1500 wakati wanafuzi wanaotozwa Sh200 wakala huyo amependekeza Sh300.
Kupitia kikao kinachotarajiwa kufanyika masaa kadhaa yajayo wadau watapata fursa ya kuhoji sababu zilizomfanya wakala huyo kupendekeza viwango hivyo kabla ya Latra kupitisha na kutangaza viwango vipya Kwa usafiri huo.