Deni Latishia Kuifilisi PSSSF



Dar es Salaam. Wakati maelfu ya wafanyakazi nchini wakisherehekea Mei mosi juzi, wadau wametoa tahadhari kwa Serikali kumaliza deni la michango ya mafao ya uzeeni kwa maelfu ya wastaafu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) lililodumu kwa miaka 23 sasa.

Kabla ya Julai mwaka 1999, Serikali ilikuwa na utaratibu wa kulipa kiinua mgongo na pensheni ya kila mwezi kupitia Hazina lakini baada ya Julai 1999 Serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) ulioanza kulipa mafao hayo mwaka 2004 baada ya kuimarika kifedha.

Hata hivyo, Serikali iliyotakiwa kuanza kupeleka michango ya wastaafu wake PSPF, haikupeleka michango na badala yake ikaomba mfuko huo kuwalipa wastaafu waliotakiwa kulipwa na Hazina kati ya Julai 1999 na 2004. Serikali iliahidi kuwa kurejesha pesa za PSPF kwa awamu lakini haikufanya hivyo miaka 23 sasa.

Kutokana na changamoto hiyo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mashirika ya Umma inashauri Serikali ikamilishe malipo ya deni lililobakia la Sh2.45 trilioni na kuandaa mikakati itakayoongeza ukusanyaji wa mapato ya michango hiyo.


Kufuatia ushauri huo, Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Dk Yahya Msigwa alisema endapo Serikali itaendelea kuchelewa kulipa deni hilo itaendelea kuhatarisha uhai wa mfuko huo.

“Kama hawatalipa mifuko itakufa na wafanyakazi watakuwa kwenye hatari ya kukosa haki zao. Athari nyingine zaidi ni kwamba Serikali itakuwa inatengeneza chuki kwa wananchi,” alisema.

Kwa mujibu wa PSSSF, jumla ya wastaafu 150,000 wanahudumiwa wakiwamo kundi la wastaafu hao wa kabla ya mwaka 1999, hatua inayosababisha mzigo wa gharama ya mafao ya pensheni ya mfuko kuzidi mapato yatokanayo na michango katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, mwaka wa fedha 2020/21 mafao yalizidi kwa Sh767bilioni, mwaka wa 2019/20 mafao yalizidi kwa Sh232 bilioni na mwaka wa fedha 2018/19 mafao yalizidi kwa Sh307 bilioni.

“Dhamana hiyo iliongeza uwezo wa mfuko hadi kufika asilimia 30 lakini bado ilikuwa chini ya asilimia 40 inayopendekezwa na PSSSF ili kuboresha zaidi uwezo wake.

“Nina shaka kuwa, kiwango kidogo cha fedha kinaathiri uwezo wa mfuko wa kulipa mafao ya pensheni kwa watumishi wa umma pindi wanapostaafu.”

Kaptain Omary Muhina, mmoja kati ya wastaafu aliyefanya kazi kwa muda serikalini kabla ya kuhamia sekta binafsi alionyesha masikitiko yake kwa wastaafu hao. “Inawaathiri wastaafu hao kisaikolojia kwa hiyo nawaonea huruma sana.”


Katika hatua nyingine Dk Msingwa alisema: “Tahadhari nyingine ni kuhakikisha wanaifanyia marekebisho ile Sheria namba 2 ya 2018 iliyounganisha mifuko yote, kwa sehemu kubwa ililalamikiwa kupunguza manufaa ya wanachama, Serikali ilitoa muda wa muaka mitano ya kujadiliana wadau.”

Dk Abel Kinyondo wa Idara ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Dar es Salaam (UDSM) alisema miongoni mwa changamoto ni pamoja na kudhoofishwa kwa vyama vya wafanyakazi licha ya kukusanya michango ya uendeshaji wake.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Hosea Kashimba aliwahi kufafanua Desemba mwaka jana kuwa Serikali imeanza kulipa deni la Sh2.17trilioni kwa PSSSF ili kupunguza mzigo gharama ya mafao ya pensheni ya mfuko ilizidi mapato yatokanayo na michango.

“Tunaipongeza Serikali kuanza kulipa deni hilo, ni hatua kubwa,” aliongeza




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad