Familia ya Mjukuu Feki wa Kibaki Yazungumza, 'Alikuwa tu Anatafuta Kazi'



Familia ya Mjukuu Feki wa Kibaki Yazungumza, Yaomba Serikali Imwachilie
Concephter Makana (kushoto) akiwa na wajomba zake Allan nyumbani kwao katika kaunti ya Bungoma, Allan Makana (kulia) akilia katika majengo ya Bunge. Picha: Tuko, Standard.
Makana aligonga vichwa vya habari mara ya kwanza mnamo Aprili 27, 2022, baada ya kupiga nduru katika Majengo ya Bunge, ambako alikuwa amekwenda kuutazama mwili wa rais wa zamani.


Mara ya pili ilikuwa Aprili 29, wakati wa misa ya wafu ya Kibaki kwenye Uwanja wa Taifa wa Nyayo, wakati Makana alipopanda jukwaani na kumwomba Askofu Mkuu Anthony Muheria ampe nafasi ya kusema neno lakini alifukuzwa na walinzi.

Concephter Makana aliwambia wanahabari kuwa mwanawe alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Kabusosi, Kanduyi, Kaunti ya Bungoma.


 
Alisema alifahamishwa kuhusu kitendo cha mwanawe na majirani kwa sababu hana televisheni na jitihada zake za kumpata kwenye simu hazikuzaa matunda.

Makana, ambaye ni kitinda mimba katika familia ya watoto wanane, alifanya mtihani wake wa KCSE mwaka wa 2015 na alipata C+.

"Mwanangu aliondoka nyumbani mwaka wa 2016 baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari mwaka wa 2015 katika shule ya upili ya Sikusi boys, aliniambia kuwa anaenda kutafuta kazi," Concephter aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake.


Mama huyo wa watoto wanane mwenye sauti nyororo alikanusha madai kwamba mwanawe ni mjukuu wa Kibaki akisema alikuwa anamuomboleza kiongozi huyo kwa kuanzisha elimu ya bure nchini ambayo alinufaika nayo.


Alisema Makana alimtaja Kibaki kama babu kama ishara ya heshima.

Concepheter alifichua kuwa alilea watoto wake pekee yake tangu mwaka 2010 wakati mumewe alipoaga dunia, na mara ya mwisho kumuona Makana ilikuwa mwaka wa 2018.

Alisema wakati huo alimtembelea na kikundi cha marafiki kutoka Pome Africa productions, shirika ambalo huigiza vitabu vya shule za upili.


 
Mama huyo alisema huenda mwanawe alifanya hivyo ili kuvutia hisia za Wakenya na kupata usaidizi wa wasamariamema kwa sababu alikuwa ametaabika Nairobi kwa miaka mingi bila kazi.

Familia ya Makana yaiomba serikali kumwachilia huru
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa wajomba wa Makana, Charles Ndumba, alisema wameshangazwa na taarifa kwamba jamaa yao anazua taharuki hadharani katika mazishi ya Kibaki akisema si mtu wa tabia hiyo.

"Hii tabia inatokana na kundi ambalo anatembea nalo. Hiyo tabia anatoa Nairobi lakini huku hakuwa na tabia mbaya," aliambia TV47.

Mjomba mwingine alifichua kuwa alizungumza na Makana kwenye simu baada ya video hizo kusambaa, na akamwambia anataka tu kuvizia umati.



"Alisema niliona ni hiyo chance ndio naweza lia labda ndio naweza pata usaidizi," alidai.

Familia hiyo iliiomba serikali kumwachilia huru Makana, ambaye alikamatwa wiki iliyopita, akitoa wito kwa wasamaria mema kumsaidia kuendelea na taaluma anayoipenda.

"Nachukua nafasi hii kwa unyenyekevu kuiomba serikali kumsamehe mtoto wetu na kumtoa rumande," Ndumba aliliambia gazeti la Star.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad